Thursday , 12th Dec , 2019

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Ilala, inamshikilia Katibu Mkuu wa Chama cha siasa cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi, kwa makosa ya kujifanya ni Ofisa wa Serikali na kuomba rushwa ya kiasi cha Shilingi milioni 50, kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya BECCO.

Katibu Mkuu wa Chama cha CCK, katikati ndugu Renatus Muabhi.

Akizungumza leo Desemba 12, 2019, Mkurugenzi wa TAKUKURU wilayani humo Christopher Myava, amesema kuwa wamemkamata Renatus Muabhi baada ya kuwekewa mtego kiwandani hapo.

"Tunamshikilia kwa kujifanya ni mtumishi wa TAKUKURU na kuomba rushwa ya Shilingi Milioni 50, kutoka kwa Mkurugenzi wa BECCO iliyoko Vingunguti, Wilaya ya Ilala, uchunguzi wetu umebaini lengo lake lilikuwa ni kuomba rushwa hiyo ili amsaidie bwana Manraj Bharya katika tuhuma zake za IPTL zinazomkabili" amesema Myava.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Juzi Desemba 10, 2019, majira ya jioni katika ofisi za kampuni hiyo akiwa tayari amekwishapokea pesa za mtego kiasi cha shilingi milioni 1, ambazo zilikuwa zimeandaliwa.