Tuesday , 14th Jan , 2020

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye ni shabiki kindakindaki wa klabu ya Simba, amehoji juu ya matumizi ya Sh. bilioni 4 alizotumia mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji 'Mo' kulipa mishahara.

Dkt.Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye tuzo za Mo Simba Awards

Hiyo imekuja kufuatia mwekezaji huyo kuamua kujiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, muda mfupi baada ya Simba kufungwa na Mtibwa Sugar katika fainali ya Mapinduzi Cup visiwani Zanzibar jana, Januari 13.

Dkt. Kingwangalla amehoji kuwa hizo bilioni nne ambazo Mo amelipa kama mishahara ndani ya klabu hiyo zimefanyika kwa makubaliano gani na kwa kujiondoa kwake katika nafasi hiyo, mishahara itaendelea kulipwaje?.

Baada ya mchezo wa fainali ya Mapinduzi Cup kumalizika kwa Simba kupoteza kwa bao moja mbele ya Mtibwa Sugar, bilionea Mo Dewji akaandika katika ukurasa wake wa Twitter ujumbe kuwa hatoendelea na nafasi yake, atabakia kama mwekezaji na nguvu kubwa ataiwekeza kwenye miundombinu na soka la vijana.