Thursday , 16th Jan , 2020

Klabu ya Yanga imepata kipigo cha kwanza kikubwa na cha kihistoria kutoka kwa Kagera Sugar kwenye ligi kuu Tanzania bara na kuendelea kushuka kwenye msimamo wa ligi.

Wachezaji na kocha wa Yanga katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar

Mchezo huo ambao ni wa kwanza chini ya kocha mpya, Luc Eymael pamoja na benchi lake la ufundi, ambapo Yanga imekubali kichapo cha mabao 3-0 katika uwanja wa nyumbani wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha wa Yanga amesema kuwa wachezaji wametengeneza nafasi nyingi kwenye mchezo huo, hali iliyopelekea kufungwa.

"Tumetengeneza nafasi nyingi kwenye mchezo wetu dhidi ya Kagera, umakini wa washambuliaji pamoja na wachezaji kumalizia nafasi hizo umetufanya tushindwe kupata matokeo chanya", amesema Eymael.

Kwa upande wa kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime amesema kuwa mbinu zake katika michezo yote sio za kujilinda na ndicho kilichowasaidia kupata ushindi katika mchezo huo. Baada ya kumalizika mchezo huo, mashabiki wa Yanga walijipanga mistari miwili kuwashangilia wachezaji wao na kuwapa moyo licha ya kupoteza. Mpaka sasa Yanga imecheza jumla ya michezo 13 na kufikisha pointi 25.

Leo ratiba ya ligi kuu itaendelea tena kwa mchezo mmoja ambapo Mbao FC itawakiribisha mabingwa watetezi Simba SC katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza. Mbao ina historia ya kufanya vizuri dhidi ya Simba hasa katika uwanja wake wa nyumbani na Simba ikitamba zaidi kwa kushinda katika uwanja wake wa nyumbani Jijini Dar es Salaam.