Sunday , 24th May , 2020

Muimbaji wa Bendi ya Kilimanjaro, Nyota Waziri, amezungumzia kifo cha Mkongwe wa Bendi hiyo Mabrouk Omar maarufu kama Mzee Njenje, na kusema kuwa alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya muda mrefu yaliyosababishwa na uzee.

Muimbaji wa Bendi ya Kilimanjaro, Nyota Waziri na kulia ni Mzee Njenje.

Hayo ameyabainisha leo Mei 24, 2020, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, ambapo pia tulizungumza na ndugu wa karibu wa Mzee Njenje na kwa pamoja walikuwa na haya ya kusema.

"Ni kweli amefariki leo Alfajiri na alikuwa anaumwa kwa muda mrefu, na juzi hapa alianza kuumwa tena, mazishi ni leo anazikwa Makaburi ya Kisutu" amesema Nyota Waziri.

Kwa upande wake ndugu wa karibu wa Mzee Njenje aliyejitambulisha kwa jina la Naima George amesema kuwa, "Alikuwa anaumwa na hali imebadilika tangu juzi, tulimpeleka Hospitali akapata huduma ya kwanza, Daktari akashauri apumzishwe kwa siku tatu, bahati mbaya leo Mungu kampenda zaidi, alipa stroke na ilimjia kama mara mbili hivi, lakini pia alikuwa anasumbuliwa na macho, figo na presha pia, ana watoto wawili na mke mmoja".

Mzee Njenje amefariki Dunia akiwa na umri wa miaka 73 na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na mara baada ya kuswaliwa utapelekwa moja kwa moja katika makaburi ya Kisutu kwa ajili ya mazishi hii leo.

Ikumbukwe kuwa Mzee Njenje, alitamba na nyimbo kama, Kinyaunyau, Kachiri, Ndembere pamoja na Boko.