Tuesday , 14th Jul , 2020

Uongozi wa klabu ya soka ya Namungo Fc, umesema licha ya wao kuwa huu ndio msimu wao wa kwanza ligi kuu,hawapendi kuona wanalinganishwa na vilabu vya KMC na Singida United ambavyo katika msimu wao wa kwanza kama wao walionyesha uhai lakini misimu iliyofuata timu hizo zimeyumba.

Wachezaji wa Namungo Fc ya Lindi wakishangilia baada ya kufunga bao katika moja ya mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.

.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa klabu hiyo ya ligi kuu, Hassan Zadadu amesema kuwa,wao Namungo ni timu inayoungwa wachimbaji wa madini kutoka mlima wa Namungo unaozalisha dhahabu ambao ni chanzo cha mapato yao hivyo si rahisi kuyumba kiuchumi kama ilivyotokea kwa Singida United.

Zadadu ameongeza kuwa,wamiliki wa timu hiyo ni wafanyakazi wa Namungo wanajitolea shilingi 200 katika kila kipato chao kinachopelekwa katika mfuko wa klabu, lakini pia wanaendelea kupigana timu ifanye vyema katika ligi kuu na pia itwae taji la FA ili wawavutie zaidi wadhamini ili kuimarisha kipato chao.

Katika hatua nyingine,Mwenyekiti huyo amesema hawatokurupuka kufanya mabadiliko ya kikosi, hadi hapo watakapopokea ripoti ya kocha wao mkuu Hitimana Thiery ambaye ndiye mwenye dira klabu hiyo ambayo ina tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa katika kombe la Shirikisho msimu ujao.

Vile vile Zadadu ameongea kwamba wanaendelea na mazungumzo ya karibu na nyota wao Bigirimana Blaise na Relient Lusajo ili wawarefushie mikataba yao na siku chache zijazo watahakikisha zoezi hilo linakamilika.

Namungo itacheza fainali ya Azam Sports Federatio Cup dhidi ya Simba August 2 mwaka huu huko mkoani Katavi,na hata wakifungwa wataiwakilisha nchi kimataifa kutokana na Simba kuwa na tiketi ya kushiriki ligi ya mabingwa Afrika kufuatia kutwaa ubingwa wa ligi kuu.

Ikumbukwe KMC katika msimu wao wa kwanza walimaliza ligi kuu katika nafasi ya 4,na kupata fursa ya kuiwakilisha nchi kimataifa kati ya timu 4 zilizopata tiketi hiyo kutoka Tanzania bara, lakini haikufika mbali na sasa inahangaika katika  ligi kuu, vile vile Singida United ilitikisa katika msimu wake wa kwanza lakini kwa sasa imeshaporomoka daraja.

.