Tuesday , 14th Jul , 2020

Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amesema kikosi chake hakikustahili kuondoka na alama tatu mbele ya Southampton katika mchezo wa ligi kuu ya England uliopigwa uwanjani Old Trafford.

Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer (Pichani) akimpa maelekezo Andreas Pereira.

 

Katika mchezo huo vilabu hivyo viwili vilitoka sare ya bao 2-2 ambapo mabao ya Manchester United yalifungwa na Marcus Rashford dakika ya 20 na Antony Martial dakika 23 huku yale ya Southampton yaliwekwa kambani na Stuart Armstrong dakika ya 12 na Michael Obafemi dakika ya 95.

Akizungumza mara baada ya mchezo kumalizika,Ole amesema walidhania wana alama tatu katika akili yao lakini ukweli ni kwamba Southampton walikua bora zaidi uwanjani, na ndio mpira ulivyo siku zote.

Man United ilikua na nafasi ya kuingia katika nafasi ya tatu kwenye ligi na kujitengeneza mazingira rafiki ya kupata tiketi ya ligi ya mabingwa Ulaya msimu ujao,lakini hivi sasa watahitaji kushinda mwechi zake tatu za mwisho zilizosalia.

United imefikisha alama 59 sawa na Leicester City ingawa vijana wa Brendan Rosgers wana wastani mzuri wa mabao,na ndio kigezo kinachowafanya washikilie nafasi ya 4 huku Chelsea wakisalia nafasi ya tatu na alama zao 60.

United itakabiliana na Crytal Palace,West Ham United na Leicester City huku Chelsea wakisalia na Norwich City,Liverpool na Wolves nao Leicester City watakipiga na Sheffield United,Tottenham Hotspurs na Manchester United.

Katika mchezo wa jana,Antony Martial alifikisha bao lake la 50 katika ligi kuu ya England,lakini pia United ilifikisha mchezo wa 18 bila ya kupoteza katika mashindano yote, wakishinda michezo 13 na sare 5.