Tuesday , 17th Nov , 2020

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare, amemuagiza Kamanda wa Polisi mkoani humo, kufanya ukaguzi wa kampuni zote za ulinzi na kutoa taarifa ndani ya miezi 3, kwa madai ya uwepo wa kampuni zinazofanya udanganyifu, ikiwemo kuajiri na kutoa silaha kwa walinzi ili hali hawawezi kuzitumia.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya jumuiya ndogondogo za kipolisi nchini, Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa, amesema kuwa makampuni hayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakifanya udanganyifu huo mara nyingi, huku wengine wakiwapa walinzi wao silaha mbovu.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Makao Makuu SACP Narcis Missama, amesema kuwa miongoni mwa jamii ndipo wahalifu walipo na hivyo suala la ulinzi shirikishi katika jamii ni jambo muhimu, ili kudhibiti masuala ya uhalifu.