
Moja ya behewa la Treni lililopata ajali mkoani Dodoma
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alipowatembelea na kuwajulia hali hospitalini hapo.
"Kipekee ninawapa pole wale wote waliopatwa na ajali hii iliyosababisha vifo na majeraha kwa wengine, serikali imeguswa na ajali hii na tuwaahidi tupo pamoja na tutaendelea kuhakikisha huduma zetu zinatolewa kwa ubora na kwa wakati", amesema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Dodoma, Gerald Maganga, alimshukuru Waziri kwa ziara hiyo na kulipongeza Shirika la Reli kwa namna walivyosaidia katika kuhakikisha walionusurika wanaendelea na safari zao.
Treni hiyo ya abiria ilipata ajali Januari 2, 2021, wakati ikiwa safarini kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea maeneo ya Tabora, Katavi (Mpanda), Kigoma na Mwanza, huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni uharibifu wa miundombinu iliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu watatu na majeruhi 66.