Friday , 19th Mar , 2021

Mabingwa wa England klabu ya Liverpool, imepangwa kucheza dhidi ya Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali kwenye droo iliyochezeshwa leo Machi 19, 2021 wakati wanafainali wa msimu uliopita Bayern Munich na PSG wamepangwa kuminyana tena.

Wachezaji wa liverpool na Real Madrid wakiwania mpira kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa ulaya

Droo hiyo imefanyika leo Machi 19, 2021 mjini Nyon nchini Uswisi, ambapo imepangwa michezo ya hatua ya robo fainali na ile ya hatua ya nusu fainali.

Katika hatua hiyo Manchester City ya England itaminyana na Borussia Dortmund ya Ujerumani, Mabingwa watatezi wa michuano hiyo Bayern Munich ya Ujerumani, watakipiga dhidi ya PSG ya Ufaransa. Timu hizi pia zilikutana kwenye mchezo wa fainali msimu uliopita na Bayern iliibuka na ushindi wa bao 1-0, na kutwaa ubingwa.

Mabingwa wakihistoria Real Madrid ya Hispania watacheza dhidi ya Liverpool ya England hii pia ni kumbukumbu ya mchezo wa fainali ya michuano hii ya msimu wa 2017-18, ambapo timu hizi zilikutana katika hatua ya fainali na Real Madrid iliibuka na ushindi wa mabao 3-1. Mabingwa wa mwaka 2004 FC Porto ya Ureno watakipiga dhidi ya mabingwa wa mwaka 2012 Chelsea ya England.

Michezo ya mkondo wa kwanza ya hatua ya robo fainali itachezwa Aprili 6 na 7 na mkondo wa pili itachezwa Aprili 13 na 14.

Na katika hatua ya Nusu fainali mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Bayern Munich na PSG atacheza na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Manchester City na Borussia Dortmund, hii itakuwa ni nusu fainali ya kwanza, Mshindi wa mchezo kati ya Real Madrid na Liverpool atacheza na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya FC Porto na Chelsea hii itakuwa ni nusu fainali ya pili, michezo ya mkondo wa kwanza itachezwa kati ya Aprili 27 na 28 na ile ya mkondo wa pili itachezwa Mei 4 na 5.

Mchezo wa fainali msimu huu utachezwa Mei 29, 2021, katika dimba la Ataturk Olympic huko Istanbul nchini Uturuki.