
Washitakiwa wa kesi ya mauaji namba 84 ya mwaka 2014, ya Alice Mtokoma (56) a wakiwa wameongozana na Polisi.
Wakisomewa shtaka la mauaji ambalo washitakiwa hao wamekabiliwa, Wakili wa serikali Andrew Mandwa na Matiko Nyangelo wakiwa katika kikao cha mahakama kuu kanda ya Iringa kilichofanyika mkoani hapa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Firmin Matogolo, wamesema watuhumiwa hao mnamo terehe 13/05/2012 walimuua kwa kumpiga marehemu Alice Mtokoma kwa kitu chenye ncha kali kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha sheria na 196 na 197 kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2019.
Wakili Matiko Nyangelo amesema kuwa siku ya tukio hilo watuhumiwa walimfuata nyumbani kwake marehemu na kumueleza kuna sehemu wanatakiwa kwenda ndipo walipofanya mauaji hayo, Amewataja washtakiwa waliohukumiwa adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa ni James Msumule, Emmanuel Ngailo, Izack Ngailo, Anitha Mbwilo na Upendo Mligo.
Amesema chanzo cha washtakiwa hao kutekeleza mauaji hayo ni kwamba mume wa Upendo Mligo ambaye ni mtoto wa Anitha Mbwilo alifariki lakini baada ya kifo hicho ndipo wawili hao walikwenda kwa mganga ili kubaini chanzo cha kifo cha kijana huyo.
Amesema baada ya kwenda kwa mganga waliambiwa kuwa aliyemuua kijana wao ni marehemu Alice Mtokoma ambaye alikuwa mke mwenzake na mshtakiwa Anitha Mbwilo.
Baada ya kupewa maelezo hayo ya mganga, ndipo Anitha na Upendo walikula njama ya kuwatafuta James Msumule, Emmanuel Ngailo na Izack Ngailo kwa kuwapatia pesa kiasi cha shilingi laki tatu ili wafanye mauaji hayo.
Kutokana na kosa hilo walilotenda washtakiwa hao, Jaji Firmini Matogolo aliwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kufuata kifungu 197 cha kanuni ya adhabu sura 16 marejeo ya 2019, ikisomwa pamoja na kifungu 322 kidogo cha kwanza na cha pili cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 marejeo ya 2019.