Saturday , 24th Apr , 2021

Ligi kuu soka Tanzania bara inaendelea leo kwa michezo miwili, mchezo wa mapema utachezwa majira ya Saa 8:00 Mchana mkoani Lindi, na mchezo mwingine utapigwa Jijini Mwanza majira ya Saa 10:00 Jioni.

Wachezaji wa Simba

Mchezo wa mapema Saa 8:00 Mchana klabu ya Namungo watakuwa wenyeji wa Mbeya City, mchezo huu utachezwa katika dimba la Majaliwa Lwangwa Lindi. Timu hizi zinatofautian alama saba kwenye msimamo wa ligi, wauaji wa Kusini Namungo wapo nafasi ya 11 wakiwa na alama 31 wakati Mbeya City wapo nafasi ya 17 wakiwa na alama 24.

Kwenye rekodi timu kizazi kipya Mbeya City haijawahi kuifunga Namungo kwenye michezo mitatu ya ligi waliokutana, wamefungwa michezo yote ukiwemo mchezo wa mkondo wa kwanza msimu huu ambao Namungo waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Na mabingwa wa Tanzania bara, Simba SC wao wapo ugenini kukipiga dhidi ya Gwambina, mchezo huu utachezwa majira ya Saa 10:00 jioni katika Dimba la Gwambina.

Gwambina wanarejea katika uwanja wao wa nyumbani baada ya kupoteza michezo yote miwili mfululizo ya ugenini waliocheza jijini Dar es salaam dhidi ya KMC na Yanga wakati Simba wamekusanya alama 6 kwenye michezo miwili ya mwisho waliocheza kanda ya ziwa baada ya kuifunga Mwadui na Kagera Sugar FC.

Mchezo wa mkondo wa kwanza ambao ulichezwa jijini Dar es salaam Septemba 26, 2020, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Katika mchezo huu Simba itawakosa wachezaji wake watatu Pascal Wawa na Luiz Miquessone wanaukosa mchezo huu kwa kutumikia adhabu ya kuwa na kadi tatu za njano wakati Thadeo Lwanga ana matatizo ya kifamialia.

Simba wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na alama 55 katika michezo 23 na endapo kama wakishinda mchezo wa leo Simba watakwea mpaka usukuani mwa msimamo wa ligi na kuwa vinara kwa tofauti ya alama moja dhidi ya Yanga wenye alama 57, wakati wenyeji wa mchezo wa leo Gambina wana alama 30 wakiwa nafasi ya 12.