Sunday , 25th Apr , 2021

Kocha wa mpira wa wavu (volleyball) Gabriel Joshua amesema kuwa maandalizi ya wachezaji wa timu za michezo mbalimbali hapa nchini yanahitajika kufanyika kwa vijana wadogo ili kupata matokeo chanya.

Timu ya Mpira wa Kikapu ya Wasichana Mkalapa wakiwa katika picha ya pamoja na Makocha wao Uwanja wa ndani wa Taifa Jijini Dar es Salaam Mara baada ya Kushika Nafasi ya Tatu,Mashindano ya Muungano Wiki iliyopita

Akizungumza kwa njia ya simu na EATV kocha huyo wa timu ya wasichana Mkalapa kutoka wilayani Masasi mkoani Mtwara amesema aliona kuna fursa ya ajira kupitia michezo hivyo akaona aanze kuwafundisha wanafunzi mpira wa wavu wakiwa katika ngazi ya shule ya msingi.

''Nilianza kuwafundisha wanafunzi wadogo wa shule ya msingi mchezo wa mpira wa wavu tangu mwaka 2006 na wanapomaliza darasa la saba huwa wanachukuliwa kwenda Sekondari ya Makongo Jijini Dar es Salaam wakiendelea kwa masomo na michezo,'' alisema kocha Joshua.

Pamoja na hilo, Kocha Joshua amesema mwaka 2015, aliona ahamishie kituo cha mafunzo cha mpira wa wavu kutoka Masasi Mjini na kukipeleka katika shule ya msingi Mkalapa iliyopo wilayani Masasi, karibu na Ndanda, mkoa wa Mtwara .

''Timu hii ya wanafunzi wa kike Mkalapa, huwa kila wanaposhiriki mashindano ya UMITASHUMITA wanashinda kwa kuwa wa kwanza, wanapata mafunzo vizuri na umri wao ni mdogo unasaidia kushika maelekezo haraka na tumewahi kushinda mashindano ya Mapinduzi kule Zanzibar mwaka huu,'' anasema Kocha Joshua.

Aidha, mwaka 2019 aliona wanafunzi wanaomaliza shule ya msingi ndani ya wilaya hiyo wasitoke kwenda nje ya wilaya bali waendelee nao kubaki katika sekondari ya Mkalapa ambapo kuna mazingira mazuri ya michezo kufundishiwa na hilo limesaidia kuimarisha timu hiyo inayoshinda kila inaposhiriki mashindando.

Baadhi ya Wachezaji wa Timu ya Wasichana Mkalapa ya Wilayani Masasi wakiwa na Makocha wao katika Viwanja vya Mkalapa Sekondari Baada ya Mazoezi,

 

Ameongeza changamoto anayoipata katika kuwakusanya wanafunzi ili wajiunge na timu hiyo ya mpira wa wavu, kuwa ni pamoja na hofu ya wazazi kuruhusu watoto wao na upatikanaji wa vifaa hasa mipira, jezi  na muda wa mazoezi kuwa ni lazima uwe baada ya masomo.

Wiki iliyopita timu ya mpira wa wavu ya Mkalapa ilishiriki mashindano ya Muungano yaliyohitimishwa Jijini Dar ea Salaam Aprili 16 wakiwa ni timu pekee ya wanafunzi kushiriki na timu za majeshi ambao ni wafanyakazi na timu hiyo kuibuka washindi wa tatu na kujizolea ushindi wa wafungaji bora na wazuiaji bora na kupata medali na vyeti.