Tuesday , 27th Apr , 2021

Watoto wawili wa familia moja ya mtaa wa Kigamboni wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, wametumbukia kwenye mto Mpanda na kupelekea mmoja kati yao ambaye jina lake ni Mariam Juma (10), kufariki dunia huku mwenzake Rehema Juma (13) akiokolewa.

Khalid Mponda, Kaka wa marehemu Mariam Juma

Akizungumza na EATV Khalid Mponda, ambaye ni kaka wa marehemu amesema sababu iliyopelekea watoto hao kwenda mtoni na mmoja kukutwa na umauti ni kutafuta mifagio waliyokuwa wameagizwa shuleni.

"Aprili 25 majira ya jioni mama yao aliwazuia wasiende kule mtoni lakini baadaye wakamtoroka, wakakutana na wenzao walikuwa kama 17 sasa wakati wanavuka wakateleza mmoja akataka kumsaidia mwenzake na wote wakawa wametumbukia kwenye mto", amesema Kaka wa marehemu.

Katika hatua nyingine kaka wa marehemu ameleeza namna walivojitahidi kumtafuta marehemu siku ya kwanza ila hakupatikana mpaka waliporudi jana Machi 26, 2021, majira ya saa 12:00 asubuhi ndiyo akapatikana.