
Kulia ni Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Ester Amos Bulaya na Kushoto ni Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso
Mhe. Bulaya amesema hayo katika kipindi cha majadiliano leo bungeni, kuhusu Wizara ya Maji ambapo amesema kama ilivyo kauli ya Waziri wa Maji, anayopenda kuitumia inayosema mtu akichezea miradi maji atamzingua, basi ndivyo wabunge watakavyomzingua endapo maji hayatatoka katika majimbo yao.
"Zibeni mianya ya upotevu wa maji kwani pesa zinapotea, wewe unasema wakikuzingua utawazingua na sisi wabunge humu ukituzingua, maji hayatoki katika maeneo yetu na sisi tutakuzingua kabla ya Rais hajakuzingua," amesema Mhe. Bulaya.
Awali akichangia hoja kuhusu Wizara ya Maji ameeleza kukinzana kwa tathimini kati ya zinazotelewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kulingana na upatikanaji wa maji nchini.
"Tujiulize hizi tathimini tunazopewa, EWURA inasema Mkuranga, Kisarawe na Chalinze upatikanaji maji ni asilimia 99, ripoti ya CAG amesema ni asilimia 53 kwa hiyo takwimu tunazopewa na Wizara na upotevu wa maji inawezekana upatikanaji wa maji nchini haufiki hata asilimia 50," amesema Mhe. Bulaya.
Wakati huo huo Mbunge wa Dodoma Mjini Mhe. Antony Mavunde ameiomba Wizara ya Maji kuangalia upya matumizi ya 'force account' katika miradi ya maji kwani imekwamisha upatikanaji wa maji kwa watanzania.
"Naiomba Wizara iangalie upya matumizi ya 'force account' ipo miradi mingi ambayo imekwama kwasababu wizara inategemea DDCA, DDCA haina uwezo wakusimamia miradi hii yote kwa wakati mmoja, naielewa sana dhana ya force account lakini kwenye miradi ya maji tuangalia kwa jicho la tofauti kwasababu wananchi wengi wanakwama na fedha zipo," amesema Mhe. Mavunde.
Sambamba na hilo Mhe. Mavunde amaemuomba Waziri Maji Mhe. Juma Aweso kutoa tamko la kuziruhusu mamlaka ambazo zina miradi hii ya maji waweze kutoka nje ya mipaka ya force account.