Saturday , 28th Aug , 2021

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amesema serikali inaendelea kuandaa mazingira wezeshi ili yasaidie timu za taifa za wanawake ‘Twiga Stars’ na ‘Tanzanite U20’ kufanya vizuri kwenye michuano yakeo mbali mbali.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Innocent Bashungwa akiongea mbele ya wanahabari kuhusu masuala ya kuboresha soka nchini.

“Sisi tutaendelea kuweka mazingira wezeshi ili muweze kujiandaa vyema kwa ajili ya mashindano mbalimbali, lakini hata huko mnako kwenda tembeeni kifua mbele mkijia kabisa Tanzania na watanzania wote wanawaamini na wako pamoja nanyi” alisema Waziri Bashungwa.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo hapo jana Agosti 27, 2021 wakati alipotembelea mazoezi ya timu hizo  katika viwanja vya Kidongo chekundu maarufu kama JK Park jijini Dar es Salaam kujionea maandalizi kabla ya mchezo dhidi ya timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini mwezi Septemba, 2021.

Akiwa katika viwanja hivyo Waziri Bashungwa pia ameongea na wachezaji wa timu hiyo akiwaleza adhima ya serikali katika kuinua michezo nchini na kuwapongeza wanamichezo wote kwa kuzidi kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa kuibuka vinara katika michezo mbalimbali.

Waziri Bashungwa amesema timu za wanawake za mpira wa miguu kwa maana ya Tanzanite na Twiga Stars zimebeba jina la Tanzania na taifa linajivunia kwa kuwa na timu hizo, ambazo mara kadhaa zimeweka historia ya kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

Kwa upande wake kocha wa timu za Taifa za wanawake Bakari Shime amemwelezea Waziri Bashungwa kuwa mashindano ya COSAFA yanayotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini yatawasaidia kujiweka vizuri kwa ajili ya maandalizi ya kuwania kufuzu mashindano ya kombe la dunia mwaka 2022.