Wednesday , 1st Sep , 2021

Atletico Madrid yamsajili tena Greizmann, Saul Niguez atimkia Chelsea, Bellerin kukipiga Real Betis wakati ambao Novack Djokovic anza kwa ushindi US Open. 'Sports Countdown' ya EA Radio ya leo Septemba 1, 2021 kuzihesabu zile sita kali za michezo kila Jumatatu hadi Ijumaa 1:15 Asubuhi.

Antoinne Greizmann akiwa na jezi ya Atletico Madrid baada ya kukamilisha usajili wake wa mkopo wa mwaka mmoja kutoka FC Barcelona.

6 - Ni idadi ya wachezaji waliotikisika kwa kusajiliwa kwenye vilabu vikubwa barani ulaya kabla ya dirisha hilo kubwa la usajili kufungwa usiku wa kuamkia leo.

Wachezaji hao ni Antoine Greizmann aliyewashtua wengi baada ya kurejea Atletico Madrid kutoka Barcelona kwa Mkopo wa msimu mmoja huku kukiwa na kipengele cha kumnunua huko baadae ilhali Saul Niguez amejiunga na Chelsea akitokea Atletico Madrid kwa mkopo wa msimu mmoja pia kukiwa na kipengele cha kumnunua mkopo huo ukimalizika.

Kiungo kinda, Eduardo Camavinga amekamlisha usajili wake wa kujiunfa na Real Madrid kwa mkataba wa miaka 6 akitokea klabu ya Rennes ya Ufaransa wakati ambao mlinzi wa kulia Nuno Mendes  (19) amejiunga na PSG kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Sporting Lisbon ya Ureno na kubadilishana na Winga Pablo Sarabia aliyetoka PSG kwenda Lisbon kwa mkopo wa msimu mmoja.

Kwa upande mwingine, Arsenal imemtoa kwa mkopo mlinzi wake Hector Bellerin kwenda Real Betis ya Hispania kwa mkopo wa mwaka mmoja na kumsajili Mlinzi Takehiro Tomiyasu (22) kutoka Bologna ya Italia na kumruhusu Winga wake Reiss Nelson kujiunga na Feyenoord ya Uholanzi kwa mkopo wa mwaka mmoja.

5 - Ni idadi ya miaka iliyopita tokea klabu ya Yanga iwe bingwa wa kombe la Shirikisho nchini ambalo kwa sasa linaitwa TFF ASFC.

Mabingwa hao wa kihistoria wà ligi kuu nchini wamemtambulisha rasmi Senzo Mazingiza Mbatha kuwa kaimu Afisa Mtendaji wao yaani CEO baada ya mzoefu huyo wa kuliongoza soka kutoka Afrika kusini kuhudumu takribani mwaka mmoja kwenye nafasi ya Ushauri wa klabu hiyo kwenye eneo maalum la kusimamia mchakato wa mabadiliko ya uendweshaji wa klabu.

4 - Ni idadi ya seti alizoshinda Nyota wa tennis anayeshika nafasi ya kwanza kwenye viwango vua ubora duniani kwa wanaume, Novak Djokovic dhidi ya kijana Mdenmark Holger Rune kwa kumfunga 6-1, 6-7, 6-2 & 6-1 na kutinga hatua ya 32 bora ya michuano ya US Open inayoendelea nchini Marekani.

Ushindi huo umezidi kumchochea Djokovic kuhusishwa kuibuka na ubingwa huo ili aweke rekodi ya kuwa mcheza tenisi wa kwanza wa wanaume kuwa na grand slam nyingi 21 na kuwa mchezaji pekee kushinda grand slam zote 4 ndani ya mwaka mmoja tokea 1969.

Djokovic sasa atacheza dhidi ya Griekspoor kwenye hatua ya 32 bora hapo kesho wakati Alexander Zverev kutoka Ujerumani ambaye ni bingwa wa Olympic kwenye tennis atacheza dhidi ya Albert Ramos-Vinolas wa Hispania kwenye hatua ya 32 bora baada ya kumtoa Sam Querrey usiku wa kuamkia leo.

3 - Ni idadi ya siku zilizopita Max Verstappen raia wa Ubelgiji awe bingwa wa mashindano ya magari ya Belgium Grand Prix yaliyofanyika nchini humo kwa kuwapiku George Russell kutoka timu ya Williams na Lewis Hamilton kutoka Mercedes kwenye ushindi uliotolewa kikanuni baada ya mbio hizo kuhairishwa kwenye mzunguko wa pili tu kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kupelekea uono hafifu kwa madereva hao.

Sasa, Rais wa shirikisho la mashindano ya magari FIA, Jean Todt usiku wa kuamkia leo amesema kamati tendaji ya shirikisho hilo litaketi October 5 mwaka huu kujadili mabadiliko ya sheria ya kumpa mtu ubingwa endapo mashindano yakihairishwa kutokana na dharula yeyote ile kwani sheria hiyo ilibezwa vikali na Lewis Hamilton.

2 - Ni idadi ya michezo ya kuwania kufuzu kucheza kombe la Dunia Qatar 2022 katika bara la Afrika itakayocheza saa 1:00 usiku wa leo Septemba 2021. Michezo hiyo ni ule utakaowakutanisha Guinea Bissau dhidi ya Guinea wakati Senegal watacheza na Togo.

Michezo mingine itakayochezwa leo ni Afrika ya Kati itacheza na Cape Verde saa 10:00 jioni, Egypt dhidi ya Angola, Libya itakipiga na Gabon wakati ambao Mali watacheza na Rwanda michezo hii mitatu kuchezwa saa 4:00 usiku wa leo.

1 - Ni idadi ya siku iliyobaki ili timu ya taifa ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars' icheze mchezo wake wa kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Qatar 2022 ambapo itacheza kesho Septemba 2 dhidi ya timu ya taifa ya DR Congo kwenye uwanja wa Lubumbashi wa timu ya TP Mazembe.

Taifa Stars imesafiri usiku wa kuamkia leo kuelekea DR Congo tayari kwa ajili ya mchezo huo huku ikitaraji kukipiga na Madagascar Septemba 7, 2021 ukiwa ni mchezo wa pili wa kundi J wa kuendelea kuwania kufuzu kombe la Dunia. Ikumbukwe Taifa Star ipo kundi moja na timu za DR Congo, Benini na Madagascar. Kila la heri Taifa Stars.