Wednesday , 29th Dec , 2021

Beki wa zamani wa Simba SC, Boniface Pawasa amesema baada ya wekundu wa msimbazi kujua wapinzani wao wa kombe la Shirikisho barani Afrika wakiwa kundi D, ameweka wazi kuwa kocha Pablo Franco anapaswa kufanya haraka kuwajua wapinzani wake ni wa aina gani.

"Ili mradi wamejua katika kundi lao wapo na nani,  wanachotakiwa kukifanya ni kuwajua wapinzani wao bila kuchelewa, kisha waanze kufanya maandalizi yanayoendana na uhalisia watakaokwenda kukutana nao,"amesema.

Simba inatarajia kukutana na kiungo wake wa zamani, Clatous Chama baada ya kupangwa kundi D na  RS Berkane ya Morocco, hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mbali na Chama ndani ya kikosi hicho, pia Simba itakutana na winga wa zamani wa Yanga, Tuisila Kisinda.
Chama aliuzwa na Simba katika klabu ya RS Berkane, ingawa hivi karibuni kulikuwepo na tetesi za kumrejesha ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi, hivyo mashabiki watamshuhudia kupitia michuano hiyo ya Caf.

Mabingwa hao wa Ligi kuu Tanzania Bara inashiriki michuano hiyo, baada ya kuanguliwa Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo iliangukia  michuano ya Kombe la Shirikisho, ambapo ilicheza na  Red Arrows ya Zambia na kuitoa kwa jumla ya mbao 4-2, ushindi uliwapeleka makundi.

Simba imepangwa kundi D na RS Berkane, Asec Mimosas na Us Gendarmerick National.