Saturday , 30th Apr , 2022

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo ametoa siku saba kwa wenyeviti wote wa Serikali za mitaa ndani ya wilaya hiyo wawe wameanzisha ulinzi shirikishi.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo

Agizo hilo amelitoa katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa Wilaya ya Temeke, Jeshi la Polisi pamoja na wenyeviti wote wa Serikali za mitaa katika wilaya hiyo ambapo kwa sehemu kubwa wamehimizwa kuanzisha polisi jamii.

 “Wenyeviti wa serikali za mitaa mlioko kwenye kikao hiki hamko hapa kwa bahati mbaya bali mmetajwa kwenye Katiba, mmetajwa kwenye Ilani ya CCM, mmetajwa katika sheria ndogo ya manispaa ya temeke na mmetajwa katika Sheria ya serikali za mitaa.Hivyo ni wajibu wetu kushiriki katika ulinzi katika meneo tunayotoka,”amesema Jokate.

Amesema kwa mujibu wa Sheria ndogo ya Halmashauri ya Wilaya ya Temeke ulinzi shirikishi ni jambo la lazima na sio utashi wa kiongozi. “Utekelezaji wa sheria hii namba 216 sheria ndogo iliyotungwa na Temeke kuhusu ulinzi shirikishi.

“Sio utashi wa kiongozi kuamua tuwe nao au  tusiwe nao, ulinzishi shirikishi lazima uwepo.Hivyo natoa siku saba mitaa isiyokuwa na ulinzi shirikishi kuitisha vikao vya dharura vya usalama na ulinzi wa mtaa waweke mkakati wa kuwa na ulinzi shirikishi.

“Pia natoa wiki moja  maeneo yenye ulinzi shirikishi lakini unasuasua lazima wachukue ya kujitathimini,”amesema Jokate na kuongeza maelekezo kwa wenyeviti wote kuhakikisha wanashiriki katika ulinzi na usalama.