Monday , 2nd May , 2022

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Amos Makala ametangaza rasmi kuanza kwa Operesheni maalumu ya kuwasaka wahalifu wanaovamia na kupiga watu majumbani maarufu kama Panya road huku akiwataka wazazi kuwa makini na watoto wao wahalifu.

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Amos Makala

RC Makalla ametoa agizo hilo huku kukiwa na taarifa za watu 19 kujeruhiwa jana katika maeneo ya Kunduchi na vijana hao wadogo.

"Leo tunawatangazia rasmi kuwa sasa tunaanzisha Operesheni kabambe ya kupambana na panya road, hatutaruhusu Panya road wakatamba na bisibisi na panga, ni wakati wa kuwaonya kuanzia leo usiku wa leo na kuendelea hakuna panya road atasalimika Dar es salaam" amesema RC Makalla.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa amewasihi wazazi wenye watoto wao wahalifu kuwa makini na vitu mbalimbali wanavyoletewa na watoto wao huku akisema wakishindwa kuwaonya basi wakawatafute katika vituo vya Polisi kuanzia kesho.

""Niwasihi wazazi kwamba Operesheni hii haitawaacha watoto wao wahalifu, kama mzazi ulizoea kupata zawadi kwa mtoto bila kujua kipato chake anakudanganya amebet kawatafuteni watoto wenu kwenye vituo vya Polisi kuanzia kesho" amesisitiza RC Makalla.

Aidha RC Makalla amewaagiza wakuu wa wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kufanya vikao na wenyeviti wote wa mitaa katika wilaya zao na ajenda ikiwa ni suala la ulinzi na usalama katika wilaya zao.

"Wenyeviti ndio wanajua ni watu wangapi wametoka jela hivi karibuni, tabia zao ni zipi, kwa siri watawapa haya mambo, na hao wenyeviti wafanye vikao na wananchi ajenda ni hiyo hiyo ya ulinzi na usalama wa maeneo yao"