Thursday , 12th May , 2022

Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi na wafuasi wake 84 ambao wanakabiliwa na kosa la kufanya mkusanyiko usio rasmi, leo hii wamekwama kusomewa maelezo ya awali ya kosa hilo baada ya kukosa ukumbi wa kuendeshea kesi hiyo.

Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi.

Ni kesi namba 12 ya mwaka 2022 inayomkabili Zumaridi na wafuasi wake 84 ambayo inaendeshwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza, imeshindwa kusomwa maelezo ya awali baada ya ukumbi uliokuwa ukitumika kutumiwa na kesi nyingine ambazo zinatolewa hukumu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Monica Ndyekobora, akaipanga kesi hiyo hadi Mei 24, mwaka huu.

Aidha katiko shtaka lingine linalomkabili Zumaridi peke yake la utoroshaji haramu wa binadamu imeahirishwa kutokana na upelelezi wake kutokamilika.

Wakili upande wa utetezi Erick Mutta, aliiomba Mahakama hiyo kuharakisha upelelezi wa shtaka la Zumaridi kufuatia mteja wake huyo kukaa rumande muda mrefu bila kesi yake ya usafirishaji haramu wa binadamu kusomwa.