
Kombe walilokabidhiwa Yanga leo kwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara
Mbeya City imewalazimisha sare timu ya wananchi kwenye mchezo ambao Yanga walitamani kupata ushindi kwakuwa ndio mchezo ambao wameutumia kukabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu. Mashabiki na wapenzi wa Yanga walitamani kuona timu yao ikishinda mchezo huu ili kuchagiza zaidi sherehe zao za ubingwa lakini wenyeji Mbeya City waligoma kuchagiza zaidi furaha kwa wananchi.
Katika mchezo huu Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake Heritier Makambo kunako dakika ya 40, lakini Mbeya City wakasawazisha bao hilo dakika ya 50 kwa njia ya mkwaju wa penati iliyopigwa na Joseph Ssemujju.
Huu ni ubingwa wa kwanza kwa Yanga baada ya misimu 4 kupita, mara ya mwisho kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ilikuwa msimu wa 2016-17. Sare ya leo imeifanya Yanga kuendeleza rekodi yake yakutopoteza mchezo wa Ligi Kuu msimu huu katika michezo 29 na wamefikisha alama 71 ukiwa umesalia mchezo mmoja kabla ya kuumaliza msimu huu.