Thursday , 15th Sep , 2022

Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila, amewataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kubadilika na kulima mazao mengine badala ya kutegemea kahawa na ndizi, maana tabia nchi inabadilika na kusababisha wakati mwingine ndizi kukosekana na kufanya uchumi wa mkoa kuyumba.

Mkuu wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila

Akizungumza katika kikao cha kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi ((CCM), wilaya ya Karagwe, Chalamila amesema kuwa Kagera haijawa na uchumi mzuri uliosimama hivyo inahitaji watu wanaoweza kutumia elimu yao kuusaidia kukua kiuchumi.

"Mkoa wa Kagera tunazalisha ndizi na kahawa, lakini ninyi ni mashahidi kwamba migomba iliyokuwepo miaka ya 80 sio tuliyonayo leo hii na ukienda vijijini hali ya utapiamlo ni kubwa kwa sababu hatuna mashamba yanayozalisha vyakula nje ya ndizi, je lishe itapatikana wapi kama samaki ni gharama kubwa, mahindi hamlimi eti mnakula ugali wakati wa njaa tu, mihogo hamtaki kula na maharage sijui kama mnakula" amesema Chalamila.

Naye mkurugenzi wa shirika binafsi la Kaderes, Leonard Kachebonao, amesema kuwa ili kuhakikisha uchumi wa mkoa unakua wamepata fedha shilingi bilioni mbili ambazo zitatumika kununua miche milioni moja ya miparachichi kwa ajili ya kuwakopesha wakulima.