Tuesday , 18th Oct , 2022

Wapalestina wameupongeza uamuzi uliochukuliwa na Australia leo wa kubatilisha hatua ya kuutambua mji wa Jerusalem Magharibi kama mji mkuu wa Israel, licha ya kukosolewa sana na Israel.

Mji wa Jerusalem Magharibi

Waziri wa masuala ya ndani ya mamlaka ya Wapalastina Hussein al Sheikh amesema kupitia ujumbe wa Twitter, wanaukaribisha uamuzi wa Australia kuhusu Jerusalem na mwito uliotolewa na nchi hiyo wa kutaka suluhisho la kuundwa madola mawili kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

Australia leo Jumanne imesema haitoutambua tena mji wa Jerusalem Magharibi kama mji mkuu wa Israel. Waziri wake wa mambo ya nje Penny Wong amesema hadhi ya mji huo inapaswa kuamuliwa kwenye mazungumzo kati ya pande mbili Israel na Palestina.

Hatua ya Australia imefuta maamuzi yaliyofikiwa mwaka 2018 na aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Scott Morrison aliyeunga mkono uamuzi uliochukuliwa na rais wa Marekani wakati huo Donald Trump.