Friday , 18th Nov , 2022

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera hasa wanaowakilisha Kata za visiwani na zile zilizoko katika mwambao wa Ziwa Victoria, wameaswa kutumia nyadhifa zao kuwataka wananchi wanaowaongoza kuacha vitendo vya uvuvi haramu maana vinaathiri uchumi wa wilaya na mkoa.

Nyavu haramu zikiteketezwa

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo, katibu tawala wilaya ya Muleba Greyson Mwengu amesema kuwa vitendo vya uvuvi haramu bado vipo na kwamba haamini kama kuna diwani anaweza kutetea viendelee kwa kisingizio cha kulinda kura zake. 

"Uvuvi ni uchumi, anayetetea hilo ajue mwisho wa siku samaki wanaweza kuisha na tukabakia na maji ya kuoga na kupikia, ikitokea hivyo wananchi watarudi kwa diwani na kumwambia hafai kwa sababu uchumi wao sio mzuri, na hawatakumbuka kama wao walisababisha hali hiyo" amesema Mwengu.

Nao baadhi ya madiwani waliozungumzia suala hilo wamekiri kuwepo kwa vitendo vya uvuvi haramu, na kwamba watu wanaojishisha na vitendo hivyo wanafanya kazi hiyo usiku wa manane, na kuiomba serikali kuongeza nguvu katika ukamataji na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kali.