Friday , 9th Dec , 2022

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kutenga kiasi cha dola za Marekani bilioni 1 zitakazotolewa kwa njia ya mkopo nafuu kwa Tanzania kupitia Mfuko wa Shirika la Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF), kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba

Kwa kipindi cha miaka mitano

Dkt. Nchemba ametoa shukrani hizo jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri anayesimamia uratibu wa masuala ya sera wa Korea Moon-Kyu Bang, alipokutana na kufanya mazungumzo naye akiwa katika ziara ya kikazi nchini.

"Septemba mwaka 2022, Tanzania na Korea tulisaini makubaliano yatakayoiwezesha Tanzania kupata mkopo wenye riba nafuu wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1, ambapo Tanzania itakopa mkopo huo kwa riba ya 0.01% kwa mwaka na kuulipa kwa kipindi cha miaka 40 ambacho kimeambatana na kipindi cha neema cha miaka 15," amesema Dkt. Nchemba

Dkt. Nchemba ameishukuru Korea kwa kuahidi pia kusaidia utekelezaji wa miradi miwili mipya ukiwemo mradi wa maji na usafi wa mazingira mkoani Iringa na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni-Zanzibar, ambayo italeta manufaa makubwa kwa wananchi.

Alisema kuwa Wizara na serikali kwa maelekezo na mwongozo wa Rais Samia Suluhu Hassan, ipo tayari kushirikiana na timu ya serikali ya Korea na wawakilishi wa Benki ya Exim nchini kuweza kukamilisha kwa haraka taratibu zote za kitaalamu ili miradi hiyo iweze kutekelezwa.

Aidha Dkt. Nchemba, amezikaribisha kampuni za Jamhuri ya Korea kuwekeza nchini, ukiwemo uwekezaji wa ubia katika miundombinu wezeshi ikiwemo ya barabara, nishati, afya, usafiri wa majini na Tehama.

Pia alibainisha kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Korea ni wa kirafiki na kindugu, ikizingatiwa kuwa serikali ya Korea iliwezesha Tanzania kupata fedha za kutekeleza miradi mingi ukiwemo mradi wa ujenzi wa daraja la Tanzanite jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Uratibu wa Sera wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Moon-Kyu Bang, ameahidi kuwa mradi wa kuboresha usambazaji maji na mazingira wa Iringa uamuzi wake wa kuutekeleza utafanyika mwishoni mwa mwaka huu na utekelezaji utaanza mara moja ilihali mradi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni  Zanzibar, taratibu za kitaalam zitakamilishwa ndani ya miezi sita ili utekelezwe. 

Vilevile ameeleza kuwa Korea inampango wa kuongeza zaidi ya marambili kiwango cha bajeti ya kutoa misaada kwa Afrika hadi kufikia mwaka 2030, hivyo ameitaka Tanzania kuandaa miradi ambayo itatekelezwa katika mpango huo utakapoanza ikiwemo miradi ya ubia na Sekta binafsi katika maeneo ya barabara, reli na mingine.