Monday , 12th Dec , 2022

Iran imesema imetekeleza mauaji ya pili yanayohusishwa na maandamano ya kuipinga serikali yanayoikumba nchi hiyo. Majidreza Rahnavard alinyongwa "hadharani" mapema Alhamisi katika mji wa Mashhad, mahakama ilitangaza

Mahakama ilimtia hatiani kwa shtaka la "uadui dhidi ya Mungu" baada ya kubaini kuwa aliwachoma kisu hadi kuwaua wanachama wawili wa kikosi cha kijeshi cha Basij Resistance Force.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuwa waandamanaji wanahukumiwa kifo kutokana na kesi zisizofuata  taratibu.

Mauaji ya kwanza kuhusiana na machafuko hayo yalifanyika siku ya Alhamisi wiki iliyopita, na kusababisha shutuma za kimataifa.

Mohsen Shekari, mwenye umri wa miaka 23, alipatikana na hatia ya "uadui dhidi ya Mungu" baada ya kupatikana amemshambulia mwanachama wa Basij kwa panga katika mji mkuu, Tehran.