Tuesday , 13th Dec , 2022

Nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi iwapo atacheza mchezo wa leo wa Nusu Fainali Kombe la Dunia dhidi ya Croatia atafikisha mchezo wake wa 25 kwenye michuano ya Kombe la Dunia na kuifikia rekodi ya gwiji wa zamani wa Ujerumani, Lothar Matthaus.

Baadhi ya mastaa wa Argentina na Croatia

Messi mwenye miaka 35, anaweza kuivuka rekodi hiyo iwapo atacheza kwenye mchezo wa fainali au kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa michuano ya Kombe la Dunia 2022 linaloendelea nchini Qatar.

Rekodi tamu kwa sasa, Argentina kwenye Nusu Fainali 4 alizocheza kwenye Kombe la Dunia hajawahi kupoteza hata mara moja,wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa magoli 6 kwa 1 dhidi ya Marekani (1930), kichapo kwa Ubelgiji cha magoli 2-0 (1986), wakiwalaza Italia kwa mikwaju ya penati 4 kwa 3 baada ya sare ya bao 1-1 na ile ya mwisho kwa kuwaondosha Uholanzi kwa mikwaju ya penati 4-2.

Wenzao Croatia wamefikia mara mbili hatua ya Nusu Fainali, mwaka 1998 walitolewa na wenyeji Ufaransa kwa kichapo cha magoli 2 kwa 1 kisha kufuzu mwaka 2018 nchini Urusi kwa ushindi wa magoli 2 kwa 1 dhidi ya England.

Argentina na Croatia wamekutana mara 5 mpaka sasa huku kila mmoja akishinda mara mbili dhidi ya mwenzake  na mara moja wakitoka sare ilhali ni mara ya 3 kukutana kwenye fainali za Kombe la Dunia huku mchezo wa mwisho ni mwaka 2018, Argentina alikubali kichapo cha magoli 3-0.