Tuesday , 20th Dec , 2022

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amesema Tanzania imepata shilingi bilioni 11.5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umahiri wa Saratani ikiwa ni mafanikio ya ziara ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Marekani

Dkt. Mollel amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao (Zoom meeting) uliowakutanisha wadau mbalimbali waliohudhuria ziara ya Rais Samia nchini Marekani

"Kwa sisi afya tumefaidi mambo mengi, la kwanza ni kituo cha umahiri wa Saratani, maana yake kinakuja kujengwa Tanzania kituo ambacho kitakuwa ni cha mfano cha standard ya Ulaya na Marekani, na hatutakuwa na sababu ya kupeleka wagonjwa wetu kule" 

"Siku ya kikao cha Rais wetu ilipatikana shilingi bilioni 11.5 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha umahiri cha Saratani, na sio mkopo ni wadau wamempenda Rais wetu wamekubali kuwekeza na hiyo ni mwanzo tu" ameeleza Dkt, Mollel
Aidha Naibu Waziri huyo amesema kuwa ziara ya Rais nchini Marekani imekuwa na manufaa makubwa ikiwemo kuleta mitaji itakayoisaidia Tanzania

"Ukiangalia kwa ujumla wake kwanini Rais Dkt. Samia amekwenda Marekani ni amekwenda kuleta mitaji, yani safari yake mwisho wa siku fedha zinakuja Tanzania ambapo zinaishia kwenye kutengeneza ajira, na kuifanya nchi yetu iwe salama"

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Marekani Dkt. Elsie Kanza ameelezea mapokezi ya Rais Samia nchini Marekani na kusema kuwa ni mazuri na wamarekani walifurahi uwepo wake na ni ishara njema katika ushirikiano wa nchi hizo

"Rais alipokelewa nchini Marekani kwa upendo, furaha na heshima kubwa sana, itoshe kusema kwamba wamarekani wanampenda sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan" 

"Uhusiano wa Tanzania na Marekani ni mzuri sana, mapokezi anayopewa Rais Dkt. Samia kila anapowasili hapa ni miongoni mwa ishara zinazoonesha uhusiano mzuri baina ya nchi hizi mbili rafiki" ameeleza Dkt. Kanza

Kuhusu faida za ushiriki wa Rais katika mikutano kadhaa iliyofanyika nchini Marekani Balozi huyo ameeleza kuwa zaidi ya makampuni 20 yameonesha nia ya kuwekeza Tanzania

"Wakati wa mkutano huo Rais alifanya mazungumzo na makampuni zaidi ya 20 ya kimarekani yenye nia ya kuwekeza Tanzania au kupanua shughuli zao nchini Tanzania" - Dkt. Elsie Kanza, Balozi wa Tanzania nchini Marekani

"Tanzania ilipokea maombi ya miadi kutoka kwa makampuni 50, makampuni mengi yaliyoomba kukutana na ujumbe wa Tanzania yanataka kuwekeza kwenye sekta za Afya, Nishati, Madini, Kilimo na TEHAMA, tunaendelea kuwasiliana nao ili kufanikisha nia yao" - amesema  Dkt. Elsie Kanza ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani
Kwa upande wa Zanzibar Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mudrik Soraga amesema moja ya mafanukio waliyoyapata ni kufanya kikao na uongozi wa kampuni kubwa ya Meta na kuahidi kuwekeza Zanzibar hivi karibuni

"Katika ziara hii tumekuwa na Mhe. Rais kila mahali na tulishiriki vile vikao vya kumkakati ikiwemo kukutana na viongozi wa Meta ambao zamani ni Facebook, na Rais alinipa fursa ya kuweza kuelezea nini ambacho tunakifanya kwa upande wa Zanzibar kwenye masuala ya Digital Transfomation"

"Wenzetu wa Meta wameonyesha utayari wao wa kuja kushirikiana na sisi kwa ajili ya kuadvance ajenda yetu ya kuhost makampuni ya TEHAMA mbalimbali kutoka Afrika kuja kuwekeza katika visiwa vyetu"

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji kituo cha uwekezaji nchini (TIC) John Mnali amesema mkutano huo umetoa fursa kwao ya kukutana na kufanya mikutano na makampuni mbalimbali kwa ajili ya kuja kuwekeza nchini 

"Kupitia mkutano huu kituo cha uwekezaji tulipata fursa ya kukutana na kampuni mbalimbali zilizoonesha nia ya kuja kuwekeza kwenye maeneo kama Kilimo, Viwanda, Madini, afya na TEHAMA"

"Kila nchi inapigania kuvutia wawekezaji kwenye nchi zao, Tanzania hatuwezi tukakaa kama kisiwa tukajifungia tukasema wawekezaji watakuja wenyewe, lazima tutoke nje tushiriki makongamano ambayo wenzetu nao wanashiriki na wanaongozana na viongozi wao"