Friday , 30th Dec , 2022

Jumla ya wananchi 4,346 kutoka katika maeneo 82 mkoani Tanga, wanatarajiwa kunufaika na mradi wa usambazaji wa umeme wa REA katika maeneo ya pembezoni mwa miji hapa nchini. 

Kushoto ni Hashim Mgandilwa Kaimu Mkuu wa Mkoa Tanga, wa pili katikati ni Hassan Said Mkurugenzi Mkuu wa REA na anayefuata ni Mrisho Masoud Mkurugenzi kampuni ya Ok Electrical

Mradi huo ambao unagharimu jumla ya shilingi bilioni 76.9 utakaotekelezwa katika mikoa nane nchini, ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 11.5 zitatumika kwa jili ya utekelezaji wa mradi huo mkoani Tanga. 

Kufuatia mradi huo wakandarasi wamesisitizwa juu ya umuhimu wa kununua vifaa kutoka kwa kampuni za ndani ya nchi ili kuimarisha uchumi wa Tanzania huku baadhi yao wakitakiwa kuacha tabia ya kununua bidhaa nchi za nje bidhaa ambazo zinapatikana hapa nchini jambo ambalo linasaidia kuimarisha uchumi wa nchi nyingine.

Kaimu Mkuu wa mkoa Tanga Hashim Mgandilwa, ameyasema hayo wakati wa makabidhiano ya mkataba wa utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme wa REA katika maeneo ya pembezoni mwa miji kwa mkandarasi kutoka kampuni ya OK ELECTICAL & ELECTRONICS SERVICE. 

"Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hasan imedhamiria kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja kwa kuweka miradi mingi ikiwemo huu uwekaji wa miundombinu ya umeme katika jamii yetu hususani maeneo ya pembezoni mwa miji kwa kuzingatia ubora wa nishati, "amesema Mgandilwa.