Friday , 30th Dec , 2022

Kocha Mkuu wa KMC FC, Thierry Hitimana, amethibitisha kuwa yupo kwenye mpango wa kukiboresha kikosi chake kwa kufanya usajili wa Wachezjai watatu, katika kipindi hiki cha Dirisha dogo la Usajili.

Hitimana amekiri kuwa katika Mchakato huo, kufuatia mapungufu yaliyojitokeza kwenye kikosi chake, kufuatia baadhi ya Wachezaji kuwa Majeruhi wa muda mrefu.

Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema tayari ameshawasilisha ripoti kwa uongozi wa juu, na ana imani watayafanyia kazi, ili wawe imara na kufanya vizuri katika michezo iliyosalia ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

“Tumecheza michezo 18 ya Ligi, tumeona madhaifu yetu na wapi tunatakiwa kuongeza nguvu, tayari nimekabidhi Ripoti kwa kutaja nafasi ninazohitaji kusajili kwa lengo la kuisaidia timu kufanya vizuri,”

“Nina imani kubwa na Viongozi wangu watafanikisha hili kwa wakati ili tuweze kuwa na kikosi kitakachoweza kupambana hadi mwishoni mwa msimu huu kwa kufikia malengo tuliojiwekea.” amesema Hitimana.

Hitimana ameongeza bado malengo ya KMC FC ni kumaliza msimu katika nafasi tano za juu, na hilo haliwezi kukamilika kama hawataboresha kikosi chao.

KMC FC inashika nafasi ya tisa katika Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa imecheza michezo 18 ikiwa na alama 22, ikishinda michezo mitano, Sare saba na imepoteza michezo sita.