Friday , 13th Jan , 2023

Elina Amos (4), mkazi wa mtaa wa Nyerere Road, Halmashauri ya mji Geita, amefariki dunia kwa kutumbukia kwemye kisima kilichopo uchochoroni wakati akitembea kuelekea dukani alipokuwa ameagizwa na mama yake majira ya saa 4:00 asubuhi ya leo Januari 13, 2023.

Kisima

Akielezea tukio hilo Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Geita Edward Lukuba, anasema mtoto huyo alitumbukia alipokuwa anapita kuelekea dukani.

"Alitumbukia kwenye kisima cha kuchotea maji ambacho kipo kwenye uchochoro wa huo mtaa wa Balenge karibia na msikitini, kifupi hiki kisima kilikuwa hakina mfuniko na rai ambayo tunaendelea kuitoa ni kwamba, visima vyote vijengewe msingi lakini pia viwekewe mfuniko," amesema Kamanda Lukuba.

Afisa Mtendaji wa mtaa huo George Maguga, amekiri tukio hilo kutokea kwenye mtaa wake ambalo limepekea kuchukua uhai wa mtoto huyo.

"Baada ya kuwa nimeona tukio hili nilipiga simu kwa OCD, na baada ya muda mfupi nikaona watu wa Zimamoto wamekuja kwa ajili ya uokozi wamemtoa mtoto na wamempeleka kwa ajili ya huduma zingine, tumeshatoa maelekezo kwamba hiki kisima sasa kifungwe kisitumike tena," amesema Maguga.