Wakizungumza kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo ya kisekta, iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hii ya Bariadi, Lupakisyo Andrea Mjukuu wa Kapange, wananchi wa Kijiji cha Mahaha, Matale, Mwadobana na Banemhi, wamesema ujenzi wa madaraja unaoshuhudiwa hivi sasa wilayani hapa unaondoa changamoto iliyowakabili wananchi tangu wakati wa uhuru.
"Nashukuru sana kuhusu daraja letu (la Mto Sandai). Watu wengi walishaenda na mto, tulikuwa tunalia sana hasa hasa sisi wanawake, watoto wa shule tunaenda hospitalishida tu, mnapelekwa na mto," amesema Tatu.
"Watu wamesombwa na maji wakiwa wajawazito wakienda Hospitali Byuna hawakuweza kuvuka wakawa wamesombwa na maji, mpaka na ng'ombe wao wakakumbwa na maji na wao wakasombwa zaidi ya 20 (watu waliosombwa na maji)" amesema Masunga.
"Katika hili daraja limetusaidia sana, tunamshukuru Mhe Samia Suluhu Hassan (Rais) kwa kutekeleza kusikiliza kilio cha wananchi," amesema Mboje.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Andrea Mjukuu wa Kapange pamoja na Mafisa wa TARURA wa wilaya hii, Khalid Mang'ola na mwenzake Hussein Mkatakweba, wamesema kukamilika kwa miundombinu hiyo itachochea maendeleo ya wananchi.
"Tunamshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia fedha za kuweza kujenga hili daraja (la Mto Sandai) Sh Bilioni 1 na 60,000. Hili daraja ni muhimu sana kwa Wilaya ya Bariadi linaunganisha kata tano, kuna Kata ya Nyakabindi, kuna Kata ya Banemhi, Kata ya Mwadobana, Kata ya Mwaubingi pale, pia kuna Kata ya Nkololo," amesema Mang'ola.
"Daraja hili (la Mto Senani) limetengenezwa kwa teknolojia ya mawe kwa gharama ya hiyo Sh Milioni 87, lakini hiyo Milioni 69 nyingine iliyobaki ndiyo iliyotumika kutengeneza barabara hii kilomita sita kwa kiwango cha changalawe," amesema Mkatakweba.
"Lakini ni miongoni mwa daraja ambayo ya mfano, ukiangalia lina milango nane lakini pia limejengwa kwa mawe. Limetengenezwa vizuri chini ya TARURA kwa hiyo ni teknolojia ambayo ni nzuri, teknolojia rahisi na wananchi wanafurahia na huku huku kuna hospitali, kuna shule, kuna sekondari upande wa huku. Kwa hiyo watu wanavuka kuja kusoma kirahisi. Kwa hiyo tunamshukuru sana Mhe Rais," amesema DC Kapange.
