Wednesday , 1st Feb , 2023

Taasisi ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Aga Khan, Tanzania (AKHST) imeingia makubaliano ya kutoa huduma za matibabu,mafunzo na uchunguzi wa afya kwa ujumla na klabu ya Azam kwa kipindi cha miaka miwili.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo, Februari Mosi, 2023 kwenye moja ya kumbi za mikutano za hospitali hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam ikiwahusisha Watendaji wakuu (CEO’s) wa taasisi zote mbili, Sisawo Konteh wa AKHST na Abdul Kareem ‘Popat’ wa Azam sambamba na viongozi wengine.

Mkataba huo unalenga kuimarisha uhusiano kati ya AKHST na Azam Fc, ukijikita zaidi kwenye kutoa huduma mbalimbali za matibabu katika vituo vyote vya AKHST vilivyopo nchini ikiwemo upimaji wa afya, upatikanaji wa huduma za maabara na mionzi,mafunzo, ukarabati na huduma za uchunguzi, uhamasishaji wa habari za afya na elimu, na mashauriano zaidi ya kitaalamu kwa wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wanaotambulika wa klabu hiyo.

Ofisa Mtendaji mkuu wa AKHST, Konteh amesema wamefurahi na kujivunia kushirikiana na Azam ikiwa ni moja ya klabu za soka zinazofanya vizuri zaidi Tanzania.

“AKHST imejitolea sana kutoa huduma za matibabu za kiwango cha kimataifa katika hospitali na Kliniki zetu huku tukiifikia jamii kwa namna mbalimbali ikiwemo kupitia michezo na afya njema

Kwa upande wa Azam, Popat amesema siku zote tunachunguza namna tunavyoweza kuimarisha afya na uchezaji wa wachezaji wetu ili kuhakikisha wanatambua uwezo wao wakiwa salama uwanjani na ushirikiano huu utatusaidia kuongeza utimamu wa mwili na afya njema kwa timu zote, Wafanyakazi na benchi la ufundi