Friday , 10th Mar , 2023

Askari wa Jeshi la Polisi kutoka Chuo cha Taaluma hiyo Dar es Salaam (DPA), wamewafariji mahabusu na wafungwa katika gereza la Segerea kwa kuongea nao na kuwapatia vitu mbalimbali lengo likiwa ni kutambua kundi hilo muhimu kwa Taifa.

Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam SACP Dkt. Lazaro Mambosasa

Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake kutoka chuo hicho SSP Anitha Semwano, amesema wanatambua umuhimu wa kundi hilo katika jamii ambapo amesema wao kama Jeshi la Polisi walitumia Siku ya Wanawake Duniani kuwapa elimu ya ukatili wa kijinsia na namna ya kutoa taarifa za ukatili katika jamii.

Aidha SSP Semwano amesema kundi hilo lipo gerezani hapo kwa mujibu wa sheria na kusema kwamba wao walikinzana na sheria za nchi na kupelekea kuwa katika mazingira hayo.

Ameeleza kuwa Jeshi hilo linatambua mchango mkubwa wa kundi hilo ambapo amebainisha kuwa kwa kutambua hilo wakufunzi wa chuo hicho pamoja na wanafunzi wa kozi ya uofisa na mkaguzi msaidizi wa polisi waliona vyema kuungana na kutoa mchango huo kwa wafungwa waliopo katika gereza hilo.

Naye Mrakibu wa Magereza SP Iyunge Saganda, amesema mchango wa askari hao utakuwa msaada mkubwa kwa wafungwa hususani wafungwa wa kike ambapo ametoa wito kwa majeshi na taasisi nyingine kuiga mfano mzuri wa Jeshi la Polisi kwa kumbuka makundi ya wahitaji.

Mkuu wa chuo hicho ambae ndiye mlezi wa Mtaandao wa Polisi Wanawake (TPF-NET) SACP Dkt. Lazaro Mambosasa amewapongeza askari hao kwa moyo wao wa kipeke wa kujali makundi maaalum.