
Mshindi wa Urais Romania Nicusor Dan
Mshindi wa uchaguzi wa rais nchini Romania, meya wa mji wa Bucharest, Nicusor Dan, amesema anatumaini kuunda serikali ya mseto itakayovijumuisha vyama vya siasa za wastani bungeni vinavyouunga mkono Umoja wa Ulaya.
Katika matamshi aliyoyatoa katika televisheni ya Romania, Dan amesema anatarajia mazungumzo ya kuunda serikali na vyama vya Social Democratic (PSD), National Liberal Party (PNL), Save Romania Union (USR) na Muungano wa
Demokrasia wa raia wa Hungary nchini Romania, (UDMR) yataendelea kwa wiki kadhaa.
Dan aidha amesema ataanza mawasiliano na makundi hayo manne yanayowakilishwa bungeni leo Jumatatu.
Kufuatia uhesabuji kura uliokumbwa na hali ya wasiwasi jana usiku, Dan, mgombea huru ambaye ni mfuasi mkubwa wa Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami NATO alimshinda mgombea wa chama cha mrengo mkali wa kulia, Alliance for the Unity of Romanians, George Simion, kwa karibu asilimia 54, ambaye alikuwa ameshinda duru ya kwanza ya uchaguzi mnamo Mei 4.