Saturday , 21st Jun , 2025

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeongeza muda wa usajili wa wanahabari kupitia Mfumo wa TAI-Habari hadi tarehe 28 Juni, 2025 ili kuwawezesha waandishi wa habari waliokamilisha usajili lakini bado hawajalipia ada ya Ithibati kufanya hivyo,

Taarifa ya Bodi hiyo imewahimiza waandishi wote wa habari nchini kutumia ipasavyo muda huu wa nyongeza kujisajili na kupata Ithibati kupitia Mfumo wa TAI-Habari ambapo Baada ya muda huo kuisha, waandishi wa habari watakaoshindwa kujisajili hawataruhusiwa kufanya kazi za kihabari, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na masharti ya Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17(1)(a), 17(2) ya Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, Tangazo la Serikali Na. 18 la mwaka 2017, wanaopaswa kujisajili ni pamoja na Waandishi wa Habari, Wahariri, Watangazaji, Wapiga Picha, Waandaaji wa Vipindi, Waandishi wa kujitegemea (Freelancers), Wanafunzi na Waandishi wa Kigeni waliokidhi vigezo vya kitaaluma katika kiwango cha elimu ya kuanzia ngazi ya Stashahada na kuendelea

Bodi inatoa onyo kali kwa mtu yeyote atakayewasilisha vyeti vya kughushi au taarifa za uongo katika mchakato wa usajili. Kitendo hicho ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika kwa mujibu wa sheria za nchi. Bodi itaendelea kuhakiki vyeti na kutoa vitambulisho kwa waandishi wa habari waliotimiza vigezo, kwa mujibu wa masharti ya Sheria hata baada ya muda wa usajili kumalizika. Usajili huu ni hatua muhimu katika mchakato wa kuanzishwa kwa Baraza Huru la Habari, kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 24 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229

Katika hatua nyingine Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imewaagiza Waajiri wa Vyombo vya Habari kuhakikisha kuwa Waandishi wa Habari wanaogombea nafasi za kisiasa wanasitisha utekelezaji wa majukumu yao ya kihabari kwa kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.

Taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) Patrick Kipangula imesema kuwa hatua hii inalenga kuzuia mgongano wa maslahi na kulinda uaminifu wa vyombo vya habari mbele ya umma, hususan katika kipindi cha uchaguzi. 

"Kwa kuzingatia uwepo wa Uchaguzi Mkuu mwaka huu, na kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 12(g) ya Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa (Tangazo la Serikali Na. 775 la tarehe 18 Septemba, 2020), waandishi wa habari ambao ni wagombea wa nafasi za kisiasa wanapaswa kuzingatia kwamba hawajihusishi katika shughuli au majukumu yoyote ya kihabari katika vyombo vya habari walivyoajiriwa kwa muda wote wa mchakato wa uchaguzi" imeeleza taarifa hiyo