Thursday , 28th Aug , 2025

“Utafiti huu utahusisha mazao ya Uvuvi aina ya Migebuka, Dagaa au Samaki wanaoelea wa tabaka la juu, ili kusaidia uwekezaji wenye tija kwa takwimu na kuvutia wawekezaji”- Dkt. Mhede

Nchi zilizopo ukanda wa Ziwa Tanganyika ambazo ni Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi, zimezindua rasmi zoezi la Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki katika Ziwa Tanganyika, ambao zoezi hilo linalenga kutambua wingi wa mazao ya Uvuvi katika Ziwa hilo.

Akizungumza katika Hafla ya Uzinduzi wa Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki Ziwa Tanganyika, jana Agosti 27, 2025 Mkoani Kigoma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede amesema Serikali imeelekeza kufanya Tathmini ya wingi wa Samaki waliopo katika Ziwa Tanganyika ili kujua wametawanyikaje na kwenye maeneo yapi, pamoja na kujua Takwimu sahihi za wingi wa Samaki katika Ziwa hilo.

“Utafiti huu utahusisha mazao ya Uvuvi aina ya Migebuka, Dagaa au Samaki wanaoelea wa tabaka la juu, ili kusaidia uwekezaji wenye tija kwa takwimu na kuvutia wawekezaji” amesema Dkt. Mhede

Aidha, Dkt. Mhede ameweka bayana kuwa zoezi hilo halifanywi tu kwa ajili ya kuandika ripoti, bali kwa ajili ya ushahidi wa kusaidia katika uundaji wa Sera, ikiwemo kujua namna ya kuendeleza Ziwa, kuhifadhi Ziwa na Rasilimali zake au matumizi ya Rasilimali hizo.

Vilevile, Dkt. Mhede amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imejipanga kikamilifu kwa kuandaa Wataalamu wa kutosha ili kuhakikisha Utafuti huo unakamilika kwa mafanikio.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh amesema, katika miaka ya Tisini Tanzania ilifanya Utafiti kama huo, na kubaini kuwa wingi wa Samaki ulikuwa ni Tani 303,645, na kwamba ongezeko la watu, mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la nguvu ya Uvuvi uenda ndio vimefanya mazao hayo kupungua kutokana na uhitaji kuongezeka zaidi.

Prof. Sheikh amesema tangu wakati huo hakuna tathmini kama hiyo ya kikanda iliyofanyika kutokana na uhaba wa rasilimali, na mwaka 1995, Tanzania ilikadiriwa kuwa tani 157,493, na iIdadi hiyo ilipungua hadi tani 144, 690 kwa mwaka 2022, na baadae ilipungua zaidi hadi tani 84,094 katika utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI).

Halikadhalika, Prof. Sheikh, amesema suala la kufanya Utafiti wa wingi wa Samaki katika Ziwa Tanganyika utasaidia kujua idadi ya Samaki waliopo katika Ziwa, ili kuweka Mipango mathubuti ya Usimamizi  wa Rasilimali za Uvuvi na kuhakikisha uendelevu.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimerei amesema Mafunzo ya Utafiti wa wingi na mtawanyiko wa Samaki katika Ziwa Tanganyika  yamefanyika kwa siku kumi, ikijumuisha kuweka sawa mitambo ya kufanyia Utafiti na kuandaa Mpango kazi wa Utafiti huo.

Pia, Dkt. Kimerei ameweka bayana kuwa Watafiti waliopata Mafunzo wataondoka kesho kwenda Burundi kwa ajili ya kuanza kazi hiyo ya Utafiti. Dkt. Kimerei amesema Utafiti huu ni muhimu kwani unasaidia katika kuhuisha Takwimu za wingi na mtawanyiko wa Samaki katika Ziwa Tanganyika na kuwezesha Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wanachama wa nchi za Ziwa Tanganyika kuweka Mikakati Madhubuti ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa hilo.