Thursday , 25th Sep , 2025

Tume ya Uchaguzi nchini Uganda imewaidhinisha Rais Yoweri Museveni na kiongozi wa upinzani Bobi Wine kugombea katika uchaguzi wa 2026 nchini humo.

Tangazo hilo linaweka mazingira ya mpambano mkali wa kisiasa kati ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81 ambaye ametawala tangu 1986 na mpinzani wake mwenye umri wa miaka 43, nyota wa pop aliyegeuka mwanasiasa ambaye anaungwa mkono na vijana wa Uganda.

Museveni, mmoja wa marais waliokaa muda mrefu zaidi barani Afrika, anawania muhula mwingine wa miaka mitano chini ya vuguvugu la National Resistance Movement.ameashiria ukuaji wa uchumi, miundombinu mipya na uthabiti kama mafanikio yake, na akiahidi kukuza uzalishaji mali, elimu, afya na vita dhidi ya rushwa.

Wakosoaji hata hivyo wanamtuhumu kwa ubabe, wakitoa mfano wa mabadiliko ya kikatiba ambayo yaliondoa ukomo wa mihula na umri, ukandamizaji dhidi ya upinzani, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Bobi Wine, ambaye alishindwa na Museveni mwaka wa 2021 uliogubikwa na madai ya udanganyifu katika kura hiyo, anasema anawakilisha kizazi kipya kinachodai mabadiliko. Kugombea kwake kulithibitishwa jana  Jumatano mjini Kampala, pamoja na mkewe katika Tume ya Uchaguzi.