Friday , 3rd Oct , 2025

Watoto na wajawazito watano walikuwa miongoni mwa waliofariki kutokana na utapiamlo mkali.

Kikundi cha matibabu cha Sudan kimeonya kuhusu kuongezeka maafa makubwa ya kibinadamu katika mji unaozingirwa wa El-Fasher baada ya watu 23 kufariki kutokana na utapiamlo mwezi Septemba, huku mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF yakiendelea kuzidisha mzozo huko Darfur.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema katika taarifa yake jana Alhamisi kwamba watoto na wajawazito watano walikuwa miongoni mwa waliofariki kutokana na utapiamlo mkali, lakini haukutoa hesabu maalum ya watoto waliofariki.

El-Fasher ndiyo ngome ya mwisho ya wanajeshi katika eneo la Darfur. Mapigano yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni, na mamia ya raia wameuawa katika mashambulizi ya Rapid Support Forces, au RSF, tangu Aprili, kulingana na ripoti ya wiki iliyopita ya Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya Mtandao wa Madaktari wa Sudan ilielezea kuzingirwa kwa mji huo na RSF kama uhalifu wa kimfumo unaowakilishwa na kuwanyima raia haki yao ya kuishi na kuwalenga raia wa El Fasher wenye njaa kama silaha ya vita.

Kundi hilo la madaktari limesema mzingiro huo ni uhalifu wa kivita dhidi ya ubinadamu chini ya sheria za kimataifa na limeilaumu jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa, kwa ukimya wake na kushindwa kuingilia kati licha ya ukubwa wa wazi wa janga hilo.

Mapigano kati ya wanajeshi na wapinzani wa RSF yalizuka mwezi Aprili 2023 na hivi karibuni yakageuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoifunika nchi, na kuua takriban watu 40,000 na wengine milioni 12 kuyahama makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa Zaidi ya watu milioni 24 wana uhaba wa chakula, kulingana na Mpango wa Chakula Duniani.

UNICEF ilisema mwezi Agosti, zaidi ya watoto 10,000 huko El-Fasher wametibiwa kwa utapiamlo mkali tangu Januari, ambayo ni mara mbili ya idadi ya mwaka jana. Katika wiki moja, angalau watu 63, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, walikufa kwa utapiamlo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto lilisema mzingiro huo ulikatiza kabisa njia za usambazaji kutoka kwa jiji hilo, na kulazimisha vituo vya afya na timu za lishe kusimamisha huduma zao na kukata matibabu kwa watoto wanaokadiriwa 6,000 walio na utapiamlo mkali.