Thursday , 9th Oct , 2025

“Pamoja na hatua ya Marekani kutangaza kuanzisha utaratibu wa dhamana za visa kwa raia wa Tanzania watakaoomba viza tajwa hapo juu, serikali inapenda kuuhakikishia umma kwamba itaendelea na majadiliano"

Serikali imethibitisha kupokea taarifa kutoka kwa serikali ya Marekani kuhusu uamuzi wake wa kuiweka Tanzania na baadhi ya mataifa mengine ya Afrika katika orodha ya nchi ambazo raia wake watatakiwa kuweka dhamana ya viza (viza bond) ili kuingia nchini Marekani kwa ajili ya shughuli za biashara (viza za B-1) au utalii (viza za B-2) kuanzia Oktoba 23 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana Oktoba 8 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema kuwa uamuzi huo umefikiwa wakati majadiliano kuhusu masuala ya uhamiaji yakiendelea baina ya Tanzania na Marekani.

“Pamoja na hatua ya Marekani kutangaza kuanzisha utaratibu wa dhamana za visa kwa raia wa Tanzania watakaoomba viza tajwa hapo juu, serikali inapenda kuuhakikishia umma kwamba itaendelea na majadiliano hayo na serikali ya Marekani kwa njia za kidplomasia ili kutafuta suluhisho lenye kuzingatia usawa, heshima na maslahi ya pande zote mbili kwa jkuzingatia uhusiano wetu mzuri uliodumu kwa zaidi ya miongo minne”, taarifa hiyo imebainisha.

Aidha, serikali imesisitiza kuwa uhusiano wake na Marekani umejengwa katika misingi ya urafiki, ushirikiano na kuheshimiana kwa muda mrefu na hivyo hatua hiyo ya Marekani haitabadilisha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza uhusiano mzuri na Marekani kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kufuata hatua hiyo, wananchi wameombwa kuendelea kufuata taratibu za kawaida za maombi ya viza kupitia ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na taarifa zaidi zitatolewa pindi mazungumzo yanayoyendelea yatakapofika hatua nyingine.