Thursday , 23rd Oct , 2025

Lissu ameieleza Mahakama kuwa shahidi huyo ana uwezo wa kutoa 'certificate' na sio 'report', na kwamba shahidi alipaswa kuandaa picha mnato (still picture) alizopelekewa kufanyiwa uchunguzi na kuzikuza, baada ya kuteuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imetoa 'uamuzi mdogo' kufuatia pingamizi lililokuwa limewekwa na mshtakiwa katika kesi ya uhaini ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu katika pingamizi lililolenga kupinga kuwasilishwa Mahakamani kama kielelezo taarifa ya uchunguzi ya picha jongefu (video), kutoka kwa shahidi wa tatu (3) wa Jamhuri Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Samwel Elibariki Kaaya.

Wakati kesi hiyo ikiendelea tena leo, Alhamisi Oktoba 23.2025, chini ya jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Danstan Ndunguru, katika kujenga hoja ya pingamizi hilo, sambamba na kufanya marejeo ya hoja mbalimbali za kisheria na kesi mbalimbali, Lissu ameieleza Mahakama kuwa shahidi huyo ana uwezo wa kutoa 'certificate' na sio 'report', na kwamba shahidi alipaswa kuandaa picha mnato (still picture) alizopelekewa kufanyiwa uchunguzi na kuzikuza, baada ya kuteuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) na au Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa mujibu wa tangazo la serikali

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Mkuu Job Mrema amepinga vikali hoja hiyo, na kuiambia Mahakama kuwa Mahakama hiyo haibanwi na maamuzi yake iliyotoa mapema jana, Oktoba 22.2025 ya kukataa kupokelewa Mahakamani hapo kwa 'Memory Card' na 'Flash Disk' kama kielelezo kutoka kwa shahidi huyo.

Mrema ameongeza kuwa mshtakiwa ameingilia 'content' ya hizo 'report' kwa kuzisoma jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya Mahakama Kuu, yanayoelekeza kwamba nyaraka yoyote haitakiwi kusomwa kabla haijawasilishwa na kupokelewa Mahakamani, hivyo kuiomba Mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo

Akijibu hoja za kutetea pingamizi lake alilokuwa ameliweka hapo jana, Lissu amesisitiza kuwa Mahakama hiyo imekataa kupokea 'Memoy Card' na 'Flash Disk' kama kielelezo, hivyo kwenye mazingira ya kisheria taarifa hiyo ya uchunguzi haiwezi kusimama yenyewe na hivyo Jaji Ndunguru amesema Mahakama imekubaliana na hoja za mshtakiwa hivyo kielelezo hicho kimekataliwa.