Zaidi ya maafisa 400 wa vyombo vya usalama pamoja na polisi wanaendelea na msako mkali wakimtafuta mshukiwa aliyehusika katika shambulio la risasi katika Chuo Kikuu cha Brown huko Rhode Island ambalo lilisababisha vifo vya wanafunzi wawili na watu wengine tisa kujeruhiwa katika shule ya Ivy League jana Jumamosi, Disemba 13, 2025.
Chuo kikuu hicho katika mji wa Providence kimesalia katika kizuizi saa chache baada ya mshukiwa aliyekuwa na bunduki kuingia katika jengo ambalo wanafunzi walikuwa wakifanya mitihani na kufanya shambulizi hilo.
Mshambuliaji huyo alitoroka baada ya kuwapiga risasi wanafunzi darasani katika jengo la uhandisi la Brown's Barus & Holley, ambapo milango ya nje ilikuwa imefunguliwa wakati mitihani ikiendelea.
Mkuu wa polisi Oscar Perez amewaambia waandishi wa habari kuwa, wapelelezi wanachunguza kwa nini eneo hilo lililengwa.
Meya wa Providence Brett Smiley amesema kuwa kwa mujibu wa maafisa wa mji huo, hawaamini kuwa kuna tishio maalum, linaloendelea kutoka kwa mshukiwa,na wamewataka wakazi wa maeneo hayo ya chuo kubaki majumbani wakati msako wa mshukiwa huyo ukiendelea.
Maafisa walitoa video ya mshukiwa huyo, mwanaume ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 aliyevalia nguo nyeusi. Naibu Mkuu wa Polisi wa Providence Timothy O’Hara alisema huenda mtu huyo alikuwa amevaa barakoa, lakini maafisa hawana uhakika.
Rais Donald Trump amewaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kwamba amefahamishwa kuhusu hali hiyo, "mbaya” na kuongeza kuwa “tunachoweza kufanya hivi sasa ni kuwaombea waathiriwa na wale ambao walijeruhiwa vibaya."


