Tuesday , 16th Dec , 2025

“Hadi sasa hatujapokea malalamiko yoyote kuhusu ongezeko la nauli. Tunawahimiza abiria kuhakikisha wanapata tiketi halali kabla ya safari ili kuepuka usumbufu,”

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limeendelea na zoezi la kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva na abiria, sambamba na kufanya ukaguzi wa magari, hususan mabasi ya masafa marefu yanayotoka nje ya mkoa, ikiwa ni juhudi za kupunguza ajali na kuhakikisha usalama wa wasafiri.

Zoezi hilo limefanyika katika Stendi ya Mabasi ya Nyegezi, ambapo Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, ACP Lwelwe Mpina, amesema lengo kuu la ukaguzi huo ni kuhakikisha magari yako katika hali nzuri ya kiusalama, madereva wanazingatia sheria za usalama barabarani na kulinda maisha ya abiria dhidi ya ajali zinazotokana na uzembe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, SSP Sunday Ibrahim, amesema ukaguzi huo ni wa mara kwa mara na ni sehemu ya operesheni endelevu ya kuhakikisha mabasi yote yanayofanya safari ndefu yanakaguliwa kabla ya kuanza safari. Ameeleza kuwa baadhi ya mabasi yalibainika kuwa na hitilafu ndogo ndogo ambazo zilitatuliwa kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari.

“Hadi sasa hatujapokea malalamiko yoyote kuhusu ongezeko la nauli. Tunawahimiza abiria kuhakikisha wanapata tiketi halali kabla ya safari ili kuepuka usumbufu,” alisema SSP Ibrahim.

Madereva wa mabasi ya masafa marefu wametakiwa kuwa na madereva wawili kwa kila safari ndefu, kudumisha nidhamu, kutumia lugha nzuri kwa abiria na kuzingatia sheria zote za usalama barabarani ili kulinda amani na usalama wa wasafiri.

Aidha, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa umma kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya usafirishaji, likisisitiza kuachana na tabia hatarishi ikiwemo mwendo kasi, kuyapita magari mengine bila tahadhari na tabia ya kukimbilia abiria, ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani.