Friday , 26th Dec , 2025

"Usiku wa leo, kwa maelekezo yangu kama Amiri Jeshi Mkuu, Marekani ilianzisha mashambulizi makali dhidi ya ISIS huko Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria, ambao wamekuwa wakiwalenga na kuwaua kwa ukatili, Wakristo wasio na hatia, katika viwango ambavyo havijaonekana kwa miaka mingi."

Marekani imefanya shambulizi dhidi ya wanamgambo wa Islamic State kaskazini-magharibi mwa Nigeria kufuatia ombi la serikali ya Nigeria, hii ni kwa mujibu wa Rais Donald Trump na jeshi la Marekani katika taarifa yake ya jana Alhamisi, Disemba 25 wakidai kundi hilo limekuwa likiwalenga Wakristo katika eneo hilo.

Katika chapisho lake la Social Truth, Rais Trump amesema, "Usiku wa leo, kwa maelekezo yangu kama Amiri Jeshi Mkuu, Marekani ilianzisha mashambulizi makali dhidi ya ISIS huko Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria, ambao wamekuwa wakiwalenga na kuwaua kwa ukatili, Wakristo wasio na hatia, katika viwango ambavyo havijaonekana kwa miaka mingi, na hata Karne!"

Kamandi ya jeshi la Marekani barani Afrika ilisema shambulio hilo lilifanyika katika jimbo la Sokoto kwa ushirikiano na mamlaka ya Nigeria na kuua wanamgambo wengi wa ISIS.

Shambulio hilo limekuja baada ya Trump mwishoni mwa Oktoba kuanza kuonya kwamba Ukristo unakabiliwa na tishio nchini Nigeria na kutishia kuingilia kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa kile alikichosema ni kushindwa kwake kukomesha ghasia zinazolenga jumuiya za Kikristo.

Kwa mujibu wa Reuters, Marekani imekuwa ikifanya safari za kukusanya taarifa za kijasusi katika maeneo makubwa ya Nigeria tangu mwishoni mwa Novemba.

Wizara ya mambo ya nje ya Nigeria imesema shambulio hilo limefanyika kama sehemu ya ushirikiano unaoendelea wa kiusalama na Marekani, unaohusisha ushirikiano wa kijasusi na uratibu wa kimkakati ili kulenga makundi ya wapiganaji.

Naye Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth katika chapisho kwenye mtandao wa X ameishukuru serikali ya Nigeria kwa msaada na ushirikiano wake na kuongeza: "Mengine zaidi yanakuja."

Serikali ya Nigeria imesema makundi yenye silaha yanawalenga Waislamu na Wakristo, na madai ya Marekani kwamba Wakristo wanakabiliwa na mateso hayawakilishi hali tata ya usalama na kupuuza juhudi za kulinda uhuru wa kidini. Lakini imekubali kufanya kazi na Marekani ili kuimarisha vikosi vyake dhidi ya makundi ya wapiganaji.