Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limethibitisha vifo vya watu wawili vilivyotokea kati ya tarehe 27 na 28 Desemba 2025 katika Wilaya ya Magu, mkoani humo, likihusisha tukio la mauaji na mtu mmoja kujiua.
Wilbert Kamata Yona (34), mfanyakazi wa Kiwanda cha Ziwa Steel na mkazi wa Kata ya Ihayabuyaga, anadaiwa kumuua mpenzi wake Marietha Benjamini Kalafala (33), mfanyakazi wa kiwanda hicho hicho na mkazi wa Mwabuyi, kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha kali kisha baadaye kujinyonga.
Tukio la mauaji ya Marietha liliripotiwa tarehe 27 Desemba 2025 majira ya saa 2:15 usiku katika Kitongoji cha Mwabuyi, Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu ambapo Marehemu aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni, mgongoni na kwenye paji la uso, kisha mwili wake kutupwa katika shamba la mahindi.
Baada ya ufuatiliaji wa kina, tarehe 28 Desemba 2025 majira ya saa 3:00 asubuhi, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa mmiliki wa nyumba ya kulala wageni iitwayo Wema, iliyopo Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu, kuwa kuna mteja amejiua kwa kujinyonga katika chumba alichokuwa amekodi.
Askari Polisi walipofika eneo la tukio, mwili ulitambuliwa kuwa ni wa Wilbert Kamata Yona, ambaye alikuwa anatafutwa kwa tuhuma za kumuua Marietha.
Miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Lugeye, Wilaya ya Magu, kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu.
Baada ya uchunguzi kukamilika, miili itakabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Jeshi la Polisi limesema chanzo cha matukio hayo ni wivu wa kimapenzi, ambapo inadaiwa Wilbert Kamata Yona alikuwa akimtuhumu Marietha Benjamini Kalafala kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi, hususan wapenzi na wanandoa, kuacha kujichukulia sheria mkononi wanapokumbana na migogoro ya kimapenzi au kifamilia, na badala yake kutafuta msaada wa ushauri kutoka kwa watu wanaowaamini, wakiwemo wataalamu wa ustawi wa jamii, viongozi wa dini au vituo vya huduma ya kisaikolojia.

