Ijumaa , 14th Sep , 2018

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa nchini (TAKUKURU), imezitaka kampuni na taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) ambazo zinawafadhili mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, kuwasilisha taarifa zao za misaada ya kifedha kutoka kwa wafadhili wao kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Julius Mbungo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Julius amesema "sisi kama taasisi ya kupambana na rushwa tutawafikia, na kama kuna ubadhirifu umefanyika basi wenye hizo NGO's waje kwetu wajisalimishe”

Katika hatua nyingine, taasisi hiyo imetangaza kumtafuta mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Simba, Zakaria Hanspope ili kujibu tuhuma za udanganyifu wa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) juu ya udanganyifu ununuzi wa nyasi bandia kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa Simba uliopo Bunju, ambapo kwa mujibu Hanspope alinunua kwa dola za kimarekani 40,577 huku bei halisi ni zaidi ya Dola za Kimarekani laki 1.

“Tumekuwa tukimtafuta kwa njia wazi, sio siri, lakini raia huyu mwenzetu haonekani sisi tunachomtaka ajitokeze ajibu tuhuma zinazomkabili na sheria zipo zitamlinda kama hana hatia na kama ana hatia sheria zitafata mkondo wake” , alioongeza Naibu mkurugenzi wa TAKUKURU.

TAKUKURU kwa sasa iko chini ya mkurugenzi mpya ambapo Septemba 6 mwaka huu, Rais Magufuli alimteua Kamishina wa Polisi, Diwani Athumani kuwa mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU akishika nafasi ya aliyekuwa mkurugenzi wa taasisi hiyo Kamishina wa Polisi, Valentino Mlowola ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Septemba 12 Rais Magufuli alimuapisha CP Diwani Athumani kuwa mkurugenzi mpya wa TAKUKURU ambapo alimpatia maagizo mbalimbali ikiwemo kupambana kikamilifu na Rushwa na kushughulika na NGOs ambazo zinaendesha shughuli zake kinyume na usajili wao.

Mtazame hapa chini Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Julius Mbungo akielezea zaidi..