Alhamisi , 16th Apr , 2015

Basi la Air Jordani lenye namba za usajili T 650 AQZ likitokea Mwanza kuelekea Arusha limepata ajali katika kijiji cha Ngonho kata ya Kitangili wilayani Nzega mkoani Tabora na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 28 kujeruhiwa vibaya.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora Suzan Kaganda.

Akizungumza na Earadio mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye ni mkuu wa wilaya ya Nzega Jackline Liana amesema mtu aliyefariki dunia amejulikana kwa jina mmoja la Emmanuel ambaye alikuwa ni fundi wa Gari hilo.

Alisema sababu ya ajari hiyo ni mwendo kasi wa dereva ambaye jina lake halikuweza kufahamika kwa haraka hata hivyo Dereva huyo alitokomea kusiko julikana baada ya kutokea ajari hiyo.

Kwa upande wake mganga mkuu mfawidhi wa Hosiptal ya Wilaya ya Nzega Erick Mbuguye alisema kuwa alipokea majeruhi 28 ambapo kati ya majeruhi wa nne hali zao ni mbaya huku mmoja akiwa amekatwa mkono kulingana na jeraha alilokuwa nalo.

Alisema kuwa hali za majeruhi wengine zinaendelea vizuri huku jitihada mbalimbali za kutoa huduma zikiendelea na kuongeza kuwa kwa wale watakao kuwa na hitaji kupelekwa katika hospitali ya rufaa watapelekwa kama itahitajika kufanyika zoezi hilo.

‘’Nimepokea majeruhi 28 na mwili mmoja lakni tunaendelea kutoa huduma na kama ikihitajika kupeleka hospital ya rufaa tutafanya lakini mpaka sasa bado na sidhani kama tutapeleka hospital ya rufaa tunaendelea kutoa huduma’’ alisema Mbuguye.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya majeruhi wamelaani vikali baadhi ya waokoaji kuwapora mali zao badala ya kutoa huduma ya uokoaji na kuongeza kuwa serikali inapaswa kutoa elimu kubwa kwa wananchi waishio pembezoni mwa barabara.

Frank Neto majeruhi akitokea jijini Mwanza kuelekea Arusha alisema kuwa baadi ya wananchi waishio pembezoni mwa barabara wamekuwa hawana uaminifu na utu kutokana na kufanya vitendo vya kupora watu mizigo yao badala ya kutoa huduma ya uokoaji katika eneo la tukio.

Akizungumzia sababu ya ajari hiyo Frank alisema sababu ni mwendo kasi wa Dereva ambaye aliyapita basi kadhaa huku akiwa katika eneo la kona ndipo gari hilo lilipo mshinda kulimuda na kujikuta likipinduka mara mbili.

‘’Kwa kweli Dereva alikuwa mwendo kasi sana alikuwa akiyapita basi kadhaa katika eneo hilo lenye kona ndipo gari likamshinda nilishtukia gari linakwenda kama mwendo ulisioeleweka, watu walipiga kelele mwenye kuomba aliomba, mwenye kulia nikashitukia gari limelia puuu’’ alisema Frenk akiwa amelala huku majeraha mengi kichwani.

Hata hivyo baadhi ya mashuhuda walisema kuwa sababu ya ajari hiyo ni kutozingatia sheria barabarani ambapo gari hilo lilikuwa mwendo kasi huku likiwa katika eneo baya lenye kona za muundo wa ‘’S’’.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Jeshi la polisi mpaka juzi watu 866 wamepoteza maisha na wengine 2,363 wamejeruhiwa kuanzia mwezi January mwaka huu hadi Machi mwaka huu ambapo ajali zilizo tokea ni 2,116 katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.

Sababu ya ajali hizo zinaelezwa ni mwendo kasi kwa baadhi ya madereva na kutozingatia sheria za barabarani ikiwa na kufutika kwa baadhi ya Alama Barabarani na kuongeza kuwa sababu nyingine ni baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhimiza mwendo kasi na baadhi ya abiria kushabikia mwendo kasi.

kamanda wa polisi mkoa wa Tabora Suzan Kaganda amethibitisha kutokea kwa ajili hiyo na kusema kwamba atatoa taarifa Rasmi kwa vyomba vya habari pamoja na majina ya watu waliojeruhiwa.