Jumatano , 10th Aug , 2016

Makundi mawili ambayo yalifuzu kushiriki hatua ya robo fainali katika shindano la Dance100% 2016 yameondolewa kushiriki katika shindano hilo kutokana na utovu wa nidhamu na kukiuka kanuni za shindano hilo.

Kundi la Best Boys Kaka zao ambalo limeondolewa ushiriki wa Dance100%

Makundi yaliyotolewa ni Best Boys pamoja na P.O.D ambayo yote yalitakiwa shiriki robo fainali ya Jumamosi tarehe 13 Agost, 2016 viwanja vya Don Bosco Osterbay Jijini Dar es salaam

Akizungumza wakati washiriki hao walipoitwa kusaini mikataba ya kushiriki shindano hilo mkuu wa matukio ya sanaa kutoka BASATA Bwana Kurwijira N. Maregesi amesema katika mashindano yoyote duniani nidhamu ni kitu muhimu sana ambacho kinaweza kumfanya mshindanaji kufika mbali katika kufanikiwa kwenye maisha na shindano.

‘’Hatuwezi kuwaita kuja kushiriki shughuli yenu na ninyi mnakuja baada ya masaa mawili baada ya tukio kuanza, tena makundi mengine yametuma mwakilishi mmoja, huu ni utovu wa nidhamu na BASATA kama msimamizi wa sanaa Tanzania hatuwezi kuvumilia jambo hili ni lazima tuoneshe mfano kwa kuwasimamisha ili wakati mwingine iwe fundisho kwa makundi mengine’’ Amesema Bwn. Maregesi.

Aidha Bwan Maregesi ameongeza kuwa lengo la makundi hayo kuitwa ni kuweza kusaini mikataba ambapo mtu mmoja hawezi kusaini mkataba wa kundi zima hivyo makundi ambayo wametuma mtu mmoja watalazimika kupisha shindano na kuacha wenye nia kuendelea.

Kwa upande wake mmoja wa Jaji wa shindano hilo Super Nyamwela amewataka washiriki wote kuheshimu muda hasa katika kipindi hiki ambacho makundi hayo yanakutana na majaji kwa ajili ya kuweza kufundishwa namna ya kutawala jukwaa, kuchagua nyimbo, pamoja na kwenda na muda.

Makundi ambayo yatashiriki Dance100% Jumamosi katika mchuano wa robo fainali Jumamosi Agusti 13, 2016 ni pamoja na
B.B.K Crew Boys , Mazebe Powder , D.D.I Crew, The Quest Crew, The Hero's Crew , Clevers Boys, Mafia Crew ,T.W.C Crew , Makorokocho Crew ,Ikulu Vegas Crew ,Wazawa Crew ,J Combat Crew.

Tags: