Chanzo kifo cha Rais Mkapa chatajwa

Jumapili , 26th Jul , 2020

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwanafamilia wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa, William Erio, imeeleza kuwa siku ya Jumatano Rais Mkapa alilazwa Hospitali baada ya kugundulika kuwa na Malaria, lakini baadaye aliaga Dunia kutokana na mshituko wa Moyo.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Marehemu Benjamin William Mkapa.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 26, 2020, wakati wa Ibada ya kuaga mwili wa Rais Mstaafu katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuwataka Watanzania kuendelea kumuenzi Rais Mkapa na kuachana na maneno ya mitandaoni ambayo yameanza kutoa taarifa za kifo chake ambazo siyo sahihi.

"Mzee wetu alikuwa hajisikii vizuri akaenda Hospitali na baada ya kuchukuliwa vipimo akakutwa na Malaria, akaanza matibabu na alilazwa siku ya Jumatano, mimi binafsi nilikuwa naye mpaka saa 2:00 usiku, baada ya kusikiliza taarifa ya habari aliinuka na akainamisha kichwa na mpaka walipokuja kumpima akawa amefariki, sababu ya kifo alipata mshituko wa Moyo" amesema William.

Aidha Erio ameeleza sababu iliyopelekea kueleza chanzo cha kifo chake, "Nilidhani ni vizuri tuliseme hivi kwa sababu kumeanza kuwa na maneno maneno kwenye mitandao, niwaombe na kuwasihi Watanzania wenzangu tumuenzi Mzee wetu aliyetangulia mbele ya haki kwa kuheshimu ukweli huo, kwamba hicho ndicho kilichosababisha kifo chake".