Uchunguzi umeanza kuhusu chanzo cha g’ombe 22 ambao ni mali ya mfugaji Alex Idege, mkazi wa Kijiji cha Kasingili, Kata ya Ilola wilayani Shinyanga, kukutwa wamekufa zizini katika mazingira ya kutatanisha.
Hatua hiyo imekuja kufuatia tamko la diwani wa Kata ya Ilola Kisena Fred ambaye amesema amesikitishwa na tukio hilo na ametaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini vifo vya mifugo hiyo ili kama ni ugonjwa hatua za haraka zichukuliwe kuudhibiti na kutoathiri mifugo ya wananchi wengine.
Kwa mujibu wa mmiliki wa mifugo hiyo majira ya saa 10 Alfajiri alisikia mifugo wakilia, akatoka nje kisha akamulika zizi akaona mifugo ipo na kurudi kulala kabla ya kuamshwa saa 11 na kijana aliyekuja kwa ajili ya kufunga ng’ombe kwenda kulima, ndipo na kuona mifugo ikiwa imekufa na kumpatia taarifa.
Amesema baada ya kupewa taarifa hiyo alikimbia tena zizini ndipo akaona ng’ombe sita wakiwa wamekufa na wengine kuzidiwa, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda waliendelea kufa hadi wakafika 22 na kubakiza ndama watatu ambao wenyewe hawakuenda malishoni.
Ofisa Mifugo Kata ya Ilola Daniel Jilala, amesema tayari wameshachukua sampuli za mifugo hiyo, na uchunguzi bado unaendelea ili kubaini chanzo cha vifo vya mifugo hiyo, lakini uchunguzi wa awali inaonyesha wamekula majani yenye sumu, uchunguzi ambao mmiliki wa mifugo hao ameukataa.
